
Kwaya ya akiba baba wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kwembe wakiimba wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka, (Picha na Vincent Mpepo).
Na Vincent Mpepo
Wakristo nchini wametakiwa kuendelea kutimiza wajibu wao katika nafasi mbalimbali ambazo Mungu amewajalia ili kumtumikia yeye na kuishi vyema katika jamii.
Wito huo umetolewa na Mtheolojia, Esther Mshana wakati akihubiri katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka Leo katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mtaa wa Kwembe na kusisitiza kuwa ufufuo wa Yesu usiadhimishwe kwa mazoea bali kuwe na upya ili uwe na maana kwa mkristo na jamii kwa ujumla.
“Kama Yesu asingefufuka kungekuwa na namna isiyoelezeka katika jambo hilo na kwamba siku hii isingekuwa na maana”, alisema Mtheolojia Esther.
Alisema ni muhimu kila mkristo kutimiza wajibu wake bila kujali changamoto anazopitia na dira yake iwe ni utimilifu wa malengo yaliyowekwa kwa utukufu wa Mungu akitolea mfano wanawake waliojihimu kwenye kaburi la Yesu ili kuupaka mwili mafuta na manukato ambao hawakukatishwa tamaa na vikwazo.
“Tusiache kutimiza wajibu wetu kwa vikwazo tunavyowekewa, badala yake tusonge mbele”, alisema Mtheolojia Esther.
Alisema wakati mwingine wakristo kama binadamu wanakatishwa tamaa na habari mbaya wanazopokea kuhusu wao wenyewe au watu wanaowahusu hivyo kutozipa nafasi habari hizo ili kazi na kusudi la Mungu litimie.
Mtendakazi katika Mtaa huo, Anna Mauki aliishukuru Kamati ya Malezi na washarika kwa namna mbalimbali wanavyofanya kazi ya Mungu hususani malezi ya watoto ambao jana walitumika kufanya uinjilishaji kupitia vyombo vya habari vya Upendo ikiwemo Redio Upendo (107.7 FM).
“Tuwekeze kwenye utumishi kwa ajili ya watoto na wala tusiwazuie katika masuala ya kikanisa”, alisema Mtendakazi Anna.
Christina Bukuku aliwajulisha washarika kuwa katika Jumapili ya kwanza ya Mwezi Mei ambapo huadhimishwa siku ya wafanyakazi duniani kutakuwa na sadaka maalumu kwa ajili ya watumishi wa Mungu mtaani hapo.
“Tuliwahi kufanya hivyo kwa miaka iliyopita na tumejisahau, Mwaka huu tuanze ule utaratibu na tuendelee nao”, alisema Christina.
Kwa upande wake, Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava aliwakumbusha washarika wa Mtaa huo kuacha ukristo wa Sikukuu na badala yake kurudi nyumbani kwa Bwana kutokana na tabia ya baadhi kuhudhuria kwenye ibada za siku za Sikukuu ikiwemo Pasaka na Noel.
“Kuhusu sadaka ya ujenzi wa Kituo cha Mimataifa cha kulelea watoto wenye mahitaji Maalumu cha Kitopeni niwaombe tuendelee nayo kama mnavyofahamu 31/05/2025 ndio kilele na Baba Askofu atakuwepo kuopkea sadaka hiyo,” alisema Mwinjilisti Mzava.
Naye, Mwenyekiti wa Ujenzi Mtaani hapo, Exaud Mchome aliwatakia heri ya Sikukuu ya Pasaka washarika wote mtaani hapo na kuwajulishwa kuwa ujenzi unaendelea vizuri.

Kwaya wa watoto wa shule ya Jumapili wakiimba katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).

Alisema wamesimama kwenye eneo la uezekaji kutokana na kusubiri foleni ya upatikanaji wa bati ambazo zilishawekewa oda na kulipiwa katika kampuni ya Alaf na kwamba zikiwa tayari muda wowote kazi hiyo itafanyika.
“Niwakumbushe tuendelee kumalizia ahadi zetu kwa awamu ya kwanza ya Januari-June 2025”, alisema Mchome.
Akielezea umuhimu wa kuwa na jengo kubwa akihusisha idadi kubwa ya washarika siku za Sikukuu ambapo wakati mwingine inaweza kuwakosesha utulivu na ufuatiliaji wa ibada kutokana na hali ya hewa kama mvua ikiwa watakaa nje kama ilivyo sasa.
Sikukuu ya Pasaka Mtaani hapo imesherehekewa kwa namna mbalimbali ikiwemo ujumbe wa neno la Mungu kupitia kwaya zote, simulizi na mistari ya moyo kutoka kwa watoto wa shule ya Jumapili na maigizo kutoka kwa akina mama wakiongozwa na Mwinjilisti Kiongozi wa Mtaa huo, Emeline Mzava.

Watoto wa Shule ya Jumapili wakihubiri kupitia simulizi katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).

Akina mama wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe ambao waliigiza wakati wa ibada ya Sikukuu ya Pasaka ambapo igizo lao liliangazia ufufuo wa Yesu Kristo. (Picha na Vincent Mpepo).

Kwaya wa watoto wa shule ya Jumapili wakiimba katika ibada ya Sikukuu ya Pasaka katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Mtaa wa Kwembe, (Picha na Vincent Mpepo).
Leave a comment