Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda akiongea na wafanyakazi na wanafunzi wakati wa ufunguzi wa kambi ya siku mbili ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa iliyoanza Leo chuni hapo. Kulia kwake ni Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho anayeshughulikia mipango, fedha na utawala, Pfofesa Josiah Katani akifuatiwa na Mkurugezi wa Rasimaliwatu Bw.Francis Badundwa, wakati kushoto ni Mratibu wa Kitengo cha Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa chuoni hapo, Dkt. Wambuka Rangi na Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukizwa Wilaya ya Bagamoyo, Rehema Kingu

Na Vincent Mpepo

Imeelezwa kuwa ulaji hovyo wa vyakula usiozingatia mlo kamili na kutofanya mazoezi ni baadhi ya visababishi vya magonjwa sugu yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Hayo yameelezwa na wataalamu wa afya waliopo kwenye kambi ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa kwa wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Kinondoni jijini Dar es salaam.

Akitoa elimu ya afya kwa wafanyakazi na wanafunzi wa chuo hicho leo, Mratibu wa Tiba Manispaa ya Kinondoni, Dkt. Omary Mwangaza alisema kutofanya mazoezi na ulaji mbovu usiozingatia makundi muhimu ya vyakula ni mojawapo ya sababu ya magonjwa sugu yasiyoambukizwa.

 “Wapo ambao wamezoea kula kila wanaposikia njaa, wakati mwingine ruhusu mwili ujile wenyewe”, alisema Dkt.Mwangaza.

Alibainisha baadhi ya tabia zenye faida kwa afya ya mwanadamu kuwa ni pamoja na kufunga, kufanya mazoezi na kupata mwanga wa jua wa asubuhi ambao una zaidi ya asilimia 85 za vitamin D zinazosaidia kutengeza kinga ya mwili.

Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukizwa Wilaya ya Bagamoyo, Rehema Kingu alisema tatizo la magonjwa yasiyoambukizwa kitakwimu linawagusa watu kwa asilimia 74 duniani, asilimia 86 katika maeneo ya ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na asilimia 34 kwa nchi ya Tanzania.

“Tumemua kuwafuata mahali walipo badala ya kuwasubiri waje hospitalini”, alisema Rehema.

Kwa upande wake, Kaimu Afisa Lishe wa Wilaya ya Bagamoyo, Flora Boniface alisema ili kuwa na mlo kamili walaji wanatakiwa kuzingatia vyakula katika makundi ya nafaka, jamii ya kunde, asili ya wanyama, mbogamboga na matunda.

“Mbogamboga zikiwekwa mafuta kiasi ni nzuri zaidi kuliko mboga isiyo na mafuta kabisa kwani ni sawa na kula makapi”, alisema Flora.

Aidha, aliitahadharisha jamii dhidi ya ulaji wa matunda mchanganyiko kwa wakati mmoja kuwa si kitu chema kifaya kwa kuwa ulaji huo unaweza kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari.

“Ulaji wa matunda kama tikiti na nanasi kwa wakati mmoja unaweza kuwa chanzo cha kisukari ikiwa mlaji hajui kiwango cha sukari katika mwili wake”, alisema Flora.

Akifungua kambi hiyo ya upimaji chuoni hapo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda alikishukuru Kitengo kinachoghulikia Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa chuoni hapo kuwa kuratibu vizuri ujuo wa wataalamu hao.

“Kila mtu anapaswa kutambua kuwa afya ndio mtaji wa kwanza na ikiwa kuna asiyetambua umuhimu na thamani ya afya njema atembelee hospitali”, alisema Profesa Bisanda.

Mratibu wa Kitengo cha Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa chuoni hapo, Dkt. Wambuka Rangi aliishukuru menejeimneti ya chuo hicho na watalaamu hao kufanikisha kambi hiyo.

Kwa mujibu wa Dkt. Rangi kambi hiyo ya upimaji ya siku mbili imeanza leo na itahitimishwa kesho kwa Dar es salaam na kwamba kitengo chake kinakusudia kuvifikia vituo vyote vya mikoa vya chuo hicho.

Mratibu wa Kitengo cha Virusi vya Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukizwa Chuo Kikuu Huria Tanzania Dkt. Wambuka Rangi akiongea na jumuiya ya wafanyakazi na wanafunzi wakati wa ufunguzi wa kambi ya siku mbili ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa iliyoanza Leo chuni hapo.

Mfamasia Lina Laiton kutoka Wilaya ya Bagamoyo akitoa huduma kwa mfanyakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Petro Sanga katika siku ya kwanza ya upimaji wa magonjwa sugu yasiyoambukizwa iliyoanza Leo chuni hapo (Picha zote na Vincent Mpepo).

Posted in

Leave a comment