
Na Gabriel Msumeno
Wanachama wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Mkoa wa Pwani wametakiwa kuweka mikakati ya kuimarisha maadili kwa watoto shuleni.
Wito huo umetolewa April 23 na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Pwani, Shangwe Twamala alipokuwa akifungua mkutano mkuu CWT Mkoa wa Pwani uliofanyika mjini Kibaha.
Twamala aliwataka walimu kutafakari namna bora za kuwafundisha na kuwashauri watoto shuleni ili shule ziendelee kuwa sehemu muhimu ya kuzalisha jamii inayotambua na kuishi katika maadili kama ilvyokuwa katika miaka ya nyuma.
“Tutafakari kuhusu maadili ya watoto tunaowalea na baadae kushauri kwenye shule zetu Ili wakue katika maadili mema kwani kwa sasa maadili yameporomoka”, alisema Twamala.
Aiidha, aliwataka walimu kuchagua kuchagua viongozi bora wenye sifa na watakaosimamia masuala ya walimu katika uongozi wao kwa kipindi cha miaka mitano.
Katibu wa CWT Mkoa wa Pwani, Susan Shesha aliishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha maslahi ya walimu katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Alisema pamoja na mafanikio hayo walimu bado wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutolipwa stahiki zao licha ya kuhakikiwa tangu Mwaka 2017.
Aliainisha changamoto hizo kuwa ni kutolipwa fedha za uhamisho, likizo na nauli huku kukiwa na walimu ambao hawajapandishwa madaraja pamoja na kukidhi vigezo.
Changamoto nyingine ni kutozingatiwa kwa mabaraza ya wafanyakazi na pia uhaba wa walimu katika shule za Msingi na Sekondari katika Mkoa huo.
Mkutano Mkuu wa chama hicho Mkoa hufanyia baada ya kufanyika mikutano mingine ngazi ya Wilaya ambayo iliambatana na uchaguzi wa viongozi.
Leave a comment