
Na Tabia Mchakama
Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) imeshiriki mahafali ya 41 ya Kidato cha sita ya Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani na kuelezea nia yake ya kuendelea kushirikiana na shule hiyo kongwe.
Akizungumza katika mahafali hayo kwa niaba ya Kamishna wa Bima Tanzania, Meneja wa TIRA Kanda ya Mashariki, Zakaria Muyengi aliupongeza uongozi wa shule hiyo na wanafunzi kwa ufaulu mzuri katika mitihani ya taifa kwa miaka mbalimbali.
Alisema TIRA itatoa msaada wa samani mbalimbali zikiwemo meza na viti kulingana na upungufu uliopo na kwamba itasaidia baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu kupata bima za afya na kusaidia ujenzi wa jengo la kulia chakula ikiwa ni changamoto zilizoainishwa.
Aidha, mamlaka hiyo iliwataka walimu, wazazi na wanafunzi kutumia bidhaa mbalimbali za bima ikiwemo bima ya maisha na bima za kawaida ili kujikinga na majanga yasiyotarajiwa na kwamba walikaribishwa katika ofisi za mamlaka hiyo kupata elimu zaidi kuhusu kuhusu masuala ya bima.

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule hiyo, Bi. Bhoke Nyagonde aliishukuru TIRA kwa ushirikiano walioonesha na msaada uliotolewa huku akibainisha kuwa malengo ya walimu katika shule hiyo ni kuongeza uzalendo na kutoa elimu bora ili kujenga wasichana wazalendo kwa taifa lao na ili wawe viongozi bora.
Moja ya mikakati ya mamlaka hiyo kutoa elimu ya bima kwa makundi mbalimbali kupitia warsha, mikutano, na semina ili kuhakikisha elimu ya bima inaufikia umma wa watanzania.
Shule ya Sekondari ya Wasichana Jangwani ni miongoni mwa shule kongwe nchini Tanzania iliyoanzishwa Mei 28, 1928 na inapatikana katikati ya jiji la Dar es salam eneo la Jangwani karibu na soko la kimataifa la la Kariakoo.

Leave a comment