
Na Vincent Mpepo
Kwa kawaida tumesikia ikizungumzwa kuwa afya bora ndio mtaji wa kwanza. Kauli hii inaangazia umuhimu wa kuwa na afya njema kwani ndiyo inakuwezesha kufanya mambo mengine ikwemo kufanya kazi au shughuli ambayo itakuingizia kipato.
Kutokuwa na afya njema husababisha mambo mengi kutoenda vyema au kukwama kwa masuala mbalimbali ikiwemo shughuli za uzalishaji, utoaji huduma na za kujiingizia kipato kama biashara, kushindwa kufanya kazi kama ni muajiriwa au hata kazi binafsi
Athari za changamoto za kiafya husababisha kushusha pato la mtu mmojammoja, familia na jamii kwa ujumla kutokana na kushuka kwa uzalishaji iwe ni kwa siku, wiki, mwezi au hata muda mrefu zaidi.

Ndio maana serikali, jamii na hata katika ngazi ya mtu mmojammoja ni muhimu kuwekeza katika afya kwa namna mbalimbali ikiwemo kuwa na bima za afya zitakazokusaidia kupata matibabu muda wowote utakapokuwa na changamoto ya kiafya, kuwekeza katika lishe bora, kufanya mazoezi na wakati mwingine kutoruhusu unywaji wa dawa za viwandani bila kufuata ushauri wa wataalamu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt. Emmanuel Mallya aliwahi kusema ni muhimu kwa jamii hususani vijana kuwekeza katika afya kwa kuwa ndio mtaji wa kwanza kabla ya vitu vingine.
Maneno ya Dkt.Malya yanaungwa mkono na Daktari Julius Mchelele kutoka Kliniki ya Path Labs jijini Dar es salaam kuwa jamii inatakiwa kujenga utaratibu wa kupima afya mara kwa mara ili kuwa na uhakika wa maendeleo ya kiafya badala ya kusubiri vipimo wakati wa homa.
Katika kuhakikisha mtu anakuwa na afya bora suala la lishe ni muhimu kwa kuwa hatupaswi kula kila kitu na wakati wote bali ni kujua unakula nini, wakati gani na kwa kiasi gani na hii inaenda sanjali na mitindo ya maisha itakayosaidia kulinda na kuimarisha kinga ya mwili.
“Wapo ambao wamezoea kula kila wanapohisi njaa, wakati mwingine ruhusu mwili ujile wenyewe”, anasema Dkt.Mwangaza.
Kumbe wakati mwingine kukaa bila kula kuna faida kwa kuwa huupa mwili namna ya kustahimili changamoto mbalimbali.
Kinga ya mwili dhidi ya magonjwa wakati mwingine himarishwa kwa aina ya mitindo ya maisha ambayo wataalamu wanashauri, kwa mfano kufanya mazoezi ambayo yataushughulisha mwili na kuzingatia mlo kamili.
Kwa mu`jibu wa Dkt. Omary Mwangaza amabye ni Mratibu wa Tiba Manispaa ya Kinondoni anasema kutofanya mazoezi na ulaji mbovu usiozingatia makundi muhimu ya vyakula ni mojawapo ya sababu ya kudhoofisha mwili zinazosababisha magonjwa sugu yasiyoambukizwa.
Dkt. Mwangaza anabainisha baadhi ya mitindo ya maisha yenye faida kwa afya ya mwanadamu ikiwemo kufunga, kufanya mazoezi na kupata mwanga wa jua wa asubuhi ambao una zaidi ya asilimia 85 za vitamin D zinazosaidia kutengeza kinga ya mwili.
Kwa mujibu wa Rehema Kingu ambaye ni Mratibu wa Magonjwa yasiyoambukizwa Wilaya ya Bagamoyo anasema tatizo la magonjwa yasiyoambukizwa kitakwimu linawagusa watu kwa asilimia 74 duniani, asilimia 86 katika maeneo ya ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara na asilimia 34 kwa nchi ya Tanzania.
Hivyo tatizo la magonjwa sugu yasioambukizwa nalo ni changamoto inayoathiri afya za watu wengi duniani, Afrika na Tanzania.
Kutokana na changamoto hiyo taasisi mbalimbali za afya za umma na binafsi zimejaribu kutafuta namna ya kuwafikia watu mahalai walipo kwa ajili ya kutoa elimu, ushauri na vipimo ili kusaida jamii.
“Tumemua kuwafuata mahali walipo badala ya kuwasubiri waje hospitalini”, anasema Rehema.
Pamoja na masuala ya asili ya namna ya kulinda afya yanayohusisha kufanya mazoezi na mengineyo suala la lishe linabaki kuwa muhimu sana katika kuhakikisha afya zinaimarika.
Mtaalamu wa lishe ambaye ni Kaimu Afisa Lishe wa Wilaya ya Bagamoyo, Flora Boniface anasema ni muhimu kwa mlaji kuwa na mlo kamili unaozingatia vyakula katika makundi ya nafaka, jamii ya kunde, asili ya wanyama, mbogamboga na matunda.

“Mbogamboga zikiwekwa mafuta kiasi ni nzuri zaidi kuliko mboga isiyo na mafuta kabisa kwani ni sawa na kula makapi”, alisema Flora.

Aidha, anaitahadharisha jamii dhidi ya ulaji wa matunda mchanganyiko kwa wakati mmoja kuwa si kitu chema kifaya kwa kuwa ulaji huo unaweza kuwa chanzo cha magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo kisukari.
“Ulaji wa matunda kama tikiti na nanasi kwa wakati mmoja unaweza kuwa chanzo cha kisukari ikiwa mlaji hajui kiwango cha sukari katika mwili wake”, anasema Flora.

Picha zote ni msaada wa akili mnemba
Leave a comment