Na Vincent Mpepo

Wanandoa wamekumbushwa kuendelea kuwa pamoja ili kuwa na umoja na mshikamano ambao ni afya kwa ustawi wa ndoa na familia kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa leo katika ibada ya Siku ya kwanza baada ya Pasaka na Mtendakazi wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kwembe, Anna Mauki wakati akihubiri kanisani hapo huku akisisitiza kuwa wapo wanandoa ambao hawana mazoea ya kuambatana pamoja kitu ambacho si chema.

Alisema ni ajabu kuwa wapo wanandoa ambao waliwahi kutembea pamoja siku ile ya ndoa yao na baada ya hapo wamekuwa wakitembea tofauti kitu ambacho bado hakimpi Mungu utukufu.

“Mnaweza kutoka na mwenza wako hata kwa gharama ndogo ili mpate muda wa pamoja”, alisema Mauki.

Alisema kwa wakristo ndoa ni agano la kudumu na kwamba katika matembezi au safari hiyo ya ndoa ni muhimu kuwa pamoja kwa kuwa ni dawa na huwasaidia kujadili mambo yanayowahusu kwa ustawi wa maendeleo yao.

Alisema matembezi ya pamoja yaanzie kwenye familia kwa kuwa wazazi na watoto wanaweza kwa pamoja wanaweza kuwa na mazungumzo ambayo ndiyo msingi katika malezi.

Aliwakumbusha wakristo waumuhimu wa kuwalea watoto katika maadili ya kikristo kwa kuwa ndio malezi bora kwa kuwa watakua wakimjua Mungu na kuwa wanajamii wema tofauti na hapo ni changamoto.

“Tuwasaidie watoto watembee katika Jina la Yesu kwa kuwa ndio njia salama”, alisema Mauki.

Aidha, aliwaasa wakristo kuacha tabia ya umbea kwa kuzungumzia watu wengine badala yake wajenge mazoea ya kuwafikishia wahusika mambo yanayowahusu.

Mwakilishi wa Ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (UKWATA) Beatrice Vales kutoka Shule ya Sekobdari ya Kwembe aliushukuru uongozi wa mtaa huo, wazazi na walezi kwa kuwawezesha kuhudhuria kongamano la Pasaka ambapo wamejifunza vitu vingi.

Beatrice Vales kutoka Shule ya Sekobdari ya Kwembe akitoa mrejesho kwa niaba ya wanafunzi wenzake kuhusu safari yao kwenye Kongamano la Pasaka, kulia na kushoto kwake ni alioambatana nao. Nyuma yao ni Mwinjiisti Kiongozi wa Mtaa huo, Bi.Emeline Mzava kushoto zaidi mwisho ni Mtendakazi Bi Anna Mauki, (Picha na Vincent Mpepo).

“Tulihudhuria na na kufundishwa masuala mbalimbali ikiwemo elimu ya uzazi, mahusiano, afya ya akili na masuala ya kujiandaa nayo kabla ya kuoa au kuolewa”, alisema Beatrice.

Aliomba washarika wa mtaa huo kuwawezesha ili wapate Mwalimu wa kwaya ili wafanye mazoezi na wakati mwingine waweze kuimba na kuonesha talanta zao kama baadhi ya shule ambazo walifanya hivyo kwenye kongamano hilo.

Mwenyekiti wa Ujenzi wa Mtaa huo, Exaud Mchome aliwajulisha washarika kuwa mabati yatakuwa tayari wiki ijayo na kwamba hatua inayofuata baada ya kuezeka ni kupiga lipu (plasta) na upakaji wa rangi ya awali (skimming).

Aliwashukuru washarika kwa sadaka hiyo na kuwaomba waendelee kumtolea Mungu ili kukamilisha ujenzi huo na kwamba awamu ya kwanza ya utoaji wa sadaka hizo itaisha Mwezi Juni 2025.

Posted in

Leave a comment