
Na Sylvester Richard
Mkuu wa Mkoa wa Singida Halima Dendego ametembelea Kaburi la Shujaa Liti ambaye ni Malkia wa kabila la wanyuturu kwa lengo la kuhamasisha utalii wa ndani.
Dendego amefanya ziara hiyo Aprili 27, 2025 akiambatana na viongozi mbalimbali vyombo vya ulinzi na usalama wakiwemo wa Jeshi la Polisi, Jeshi la Magereza na Zimamoto na Uokoaji.

Akiwa kaburini hapo amewahamasisha wananchi wa Mkoa huo na wageni wanaofika kusherehekea maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani (Mei Mosi) kutemebelea kwenye kaburi la Shujaa huyo Mwanamke lililopo katika Kijiji cha Makuyu Singida
“Mnakaribishwa kutemebelea maeneo mengine ya kihistoria yakiwemo makazi ya Mtemi Senge na Ziwa Kinda maeneo ambayo yanapatikana Manispaa ya Singida”, alisema Dendego.
Alitumia fursa hiyo kuwaelekeza wananchi kumuenzi Shujaa Liti kwa kushiriki uchaguzi Mkuu 2025 na kuchagua viongozi bora huku pia akihaidi kujenga Chuo cha Nyuki kando ya Kaburi la Liti kwakuwa Malkia huyo alipambana na wakoloni wa Kijerumani kwa kutumia nyuki.
Shujaa Liti alizaliwa mwaka 1860 na kufariki mwaka 1907 baada ya kukatwa kichwa na wakoloni wa Kijerumani ambao waliondoka na kichwa hicho hadi sasa ambapo Mkuu huyo wa Mkoa ameahidi kufuatilia kichwa hicho kirejeshwe kama kama kilivyorejeshwa cha Shujaa Mkwawa.

Leave a comment