
Na Annamaria John
Serikali itaendeleza ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuwa na mfumo madhubiti wa kusimamia miradi ya maji hususani katika maeneo ya vijijini kwa kushirikiana na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Alex Tarimo wakati wa kikao kazi kati ya wizara yake na taasisi ya kidini ya Kanisa la Anglikana jijini Dodoma walipokwa wakijadili mfumo wa utekelezaji wa miradi ya maji inayotekelezwa na Taasisi hiyo katika mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara.
“Mfumo huu wa kushirikisha wadau ni pamoja na kutimiza azma ya serikali ya kufikisha huduma ya maji kwa wananchi kwa asilimia 85 vijijini na 95 mjini “, alisema Tarimo.
Aidha alisema lengo la kikao hicho ni kuendelea kushirikisha sekta binafsi katika kufikisha huduma endelevu ya maji bila kikwazo kwa wananchi.
Kiongozi wa taasisi hiyo Padre.Godfrey Monjera amesema pamoja na jitihada wanazofanya kufanikisha miradi hiyo bado uhitaji wa huduma ya maji upo.
“Sisi kama taasisi ya kidini tumekuwa tukishughulika na miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya maji,lakini bila kushirikiana na serikali tusingeona matokeo mazuri” alisema Padre Monjera.

Leave a comment