Viziwi Hupenda Kuitwa Hivyo Badala ya Wasiosikia

Na Vincent Mpepo        

Imebainika kuwa jamii ya viziwi wanapenda kuitwa viziwi badala ya kuitwa wasiosikia au namna nyingine kwa kuwa majina mengine kuwarejelea wao huwa na maana zenye ukakasi na wakati mwingine kuwa na maana mbaya kitu ambacho si sawa.

Hayo yamebanishwa na Mkufunzi wa Chuo Cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Malise Swila wakati wa mafunzo ya Siku moja ya Lugha ya Alama yaliyofanyika Leo jijini Dar es salaam na kuhusisha wahadhiri, watumishi waendehaji na mafundi, wakufunzi, viziwi na jamii ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Malisa alisema kimsingi viziwi hawapendi kuitwa majina mengine kwa kuwa majina hayo hayana uhalisia na wakati mwingine yanabeba tafsiri mbaya kuelezea hali hiyo na kuishauri jamii kuwaita viziwi kwa kuwa ni jina wanalolipenda.

“Kwa mfano mkituita wasiosikia au bubu mnatukosea na ina tafsiri tofauti na tulivyo”, alisema Malise

Mkalimani wa Lugha ya Alama ambaye ni mtumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Janet Phillip alisema madhumuni ya semina hiyo kujaribu kupunguza vizingiti vya kimawasiliano kati ya viziwi na wafanyakazi wa chuo hicho ili kuhakikisha wanapata huduma stahiki.

“Semina hii ni muhimu kwa kuwa kuna kundi la watu ambao tunawaacha nyuma kwa sababu ya lugha ili kurahisha utoaji wa huduma”, alisema Janet

Alisema jamii ya viziwi wana changamoto mbalimbali na wakati mwingine inawawia vigumu kuwasilisha changaoto hizo kutokana na watumishi kutoelewa lugha ya alama hivyo imekuwa muhimu ili walao kupata maarifa ya awali ya namna ya kuwasiliana kati ya viziwi na watumishi.

Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Mtaalamu wa Isimu na Lugha ya alama, Julius Taji alisema ni muhimu kwa jamii kuifunza namna mbalimbali za mawasiliano ili kurahisisha mawasiliano na viziwi katika jamii zetu ikiwa lugha ya alama itashindikana.

“Tunapaswa kujua mwasiliano ya jumla yanayojumuisha mbinu zozote zitazakosaidia kiziwi kuelewa na kupata ujumbe ili apate mahitaji yake”, alisema Dkt.Taji

Akifunga semina hiyo kwa niaba ya Mtiva wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii, Dkt.Halima Kilungu ambaye ni Mkuu wa Idara ya Jiografia, Utalii na Ukarimu alisema semina hiyo ni muhimu sana kwa kuwa waliohudhuria wamepata maarifa tofauti na walivyokuja.

“Nimegundua kuwa uwepo wa taa katika majengo yetu iwe kwenye huduma au majumbani ni muhimu kwa kuwa ni mwanzo mzuri wa kurahisha mawasiliano na viziwi”, alisema Dkt.Kilungu

Alisema katika sekta ya utalii na ukarimu kuna changamoto za kimawasiliano kwa watalii viziwi kutokana na waongoza watalii kutokufahamu lugha ya alama na anadhani ni eneo linaloweza kufanyiwa kazi ili kuendelea kuwavutia watalii kutemebelea vivutio vya utalii hata kama ni viziwi.

Posted in

Leave a comment