
Na Vincent Mpepo
Vyombo vya habari vya runinga nchini vimetakiwa kuajiri wakalimani wa lugha ya alama wanaotambua wajibu wao katika kazi ya ukalimani ili kuepusha upotoshaji wa maudhui ya taarifa wazitoazo kwa kufahamu au kutofahamu hivyo kuathiri upatikanaji wa tafsiri sahihi kwa jamii ya viziwi.
Hayo yamebanika katika semina ya siku moja ya kujenga uelewa wa lugha ya alama iliyofanyika jana katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar es salaam na kuhusisha jamii ya viziwi, wahadhiri, wakufunzi na watumishi wa chuo hicho, Chuo Kikuu cha Dar es salaam na Chuo cha Elimu Maalumu Patandi.



Mkufunzi wa Chuo Cha Ualimu Elimu Maalumu Patandi, Malise Swila alisema baadhi ya vyombo vya habari vya runinga nchini vimeajiri wakalimani ambao hawaeleweki au wakati mwingine kutoa tafsiri zisizo sahihi au kuleta makelele kwa viziwi wanaofuatilia taarifa mbalimbali katika vyombo hivyo.

Alisema ni muhimu kwa wakalimani wanaoajiriwa kutambua kuwa wanahudumia kundi muhimu na kwamba makosa madogomadogo wanayofanya yanaathiri kundi la viziwi kupata ujumbe mujarabu.
“Mkalimani katika runinga ni lazima awe mesomea na aweze kukalimani katika miktadha na matukio husika ili kutoa tafsiri sahihi”, alisema Malise
Alisema ikiwa mkalimani ukalimani katika miktadha ya kanisani, msikitini au maeneo ya tiba ni vyema akazingatia mavazi na rangi ambazo hazitaleta ukakasi kwenye tafsiri kwa hadhira husika na kwamba mavazi ya wakalimani na rangi za nguo wavaazo zina athari sana katika tafsiri kwa hadhira ya viziwi ambapo wakati mwingine kutokana na mwanga huwa ni kelele machoni pao.
Alisema wapiga picha wa runinga wanapaswa kujua maeneo ya mwili yanayotambulika katika kufanikisha lugha ya alama kwa viziwi ili kuleta maana inayokusudiwa na kwamba ujazo wa picha na makini ya hadhira inapaswa kuelekezwa kwenye eneo la juu katika mwili wa mkalimani kuanzia kiunoni kupanda juu na si vinginevyo.
Alisema walao Kituo cha Runinga cha Azam kinazingatia maoni yao na kufanyia kazi katika eneo la ukalimani tofauti na vituo vya Runinga za TBC na ITV.
Kaimu Mtiva wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii, Dkt.Henry Mambo alisema Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni taasisi ya umma ambayo inatoa elimu kwa watu wa makundi yote ikiwemo viziwi na kwamba wanatambua kuwa kundi la viziwi kama yalivyo Makundi mengine linahitaji kupata huduma hizo ili kurahisha mawasiliano.
“Hatahivyo semina hii ni utekelezaji wa mpango mkakati wa chuo katika kutimiza wajibu wake kwa umma”, alisema Dkt.Mambo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Teknolojia na Huduma Mikoani, Profesa Leonard Fweja alisema chuo chake ni mdau muhimu kwa watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo viziwi na kwa kutambua hilo wanashirikiana na wadau wengine ili kupata matokeo mazuri na makubwa zaidi.
Alisema chuo chake kimehusika katika kuandaa, kuratibu na kuwa mwenyeji wa semina hiyo kwa kutambua umuhimu wa mawasiliano katika maisha ya kila siku kwa watu wa makundi yote ikiwemo viziwi.
Mhadhiri wa Mawasiliano na Lugha ya Alama kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Justin Msuya ambaye ni mmoja wa wawezeshaji katika semina hiyo alizungumzia umuhimu wa kutambua njia zinazosaidia jamii kupata makini ya viziwi ili kufanya mawasiliano nao kuwa ni kwa kumwangalia, kumgusa begani, kugonga meza na wakati mwingine kutumia miguuu kwa kukanyaga chini.
“Mambo mengine ya kuzingatia ni matumizi ya sura, mwili na umbali kati yako na kiziwi”, alisema Dkt.Msuya.

Alisema lugha ya alama ina sifa kama zilivyo lugha nyingine ikiwemo kutohoa na inazingatia utamaduni wa eneo husika.

Leave a comment