
Na Farida Mkumba, Dodoma
Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) kimeendesha mafunzo maalumu kwa watumishi wake kwa lengo la kuboresha utendaji kazi na kuongeza ufanisi katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
Mafunzo hayo yamefanyika leo katika ukumbi wa Maktaba ya Chuo, Kampasi Kuu Hombolo, yakiwahusisha watumishi kutoka Kampasi ya Hombolo na ile ya Dodoma mjini.
Miongoni mwa mada zilizowasilishwa ni pamoja na “Namna ya Kukabiliana na Msongo wa Mawazo Kazini”, iliyotolewa na Dkt. Garvin Kweka, Mtaalamu wa magonjwa ya figo kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Mada nyingine zilihusu matumizi ya mfumo wa ndani wa upimaji utendaji kazi wa watumishi, na mbinu za utoaji wa huduma bora kwa wateja.
Zaidi ya watumishi 200 wameshiriki mafunzo hayo, yakiongozwa na Mkuu wa Chuo, Dkt. Lameck Mashala, ambaye aliwataka washiriki kuyatumia mafunzo hayo kama nyenzo ya kuongeza tija katika utumishi wa umma.

Leave a comment