
Na Vincent Mpepo
Watalaamu wa lugha wameonya kuwa sera za lugha zinazotumika katika nchi nyingi za Afrika zimekuwa kikwazo kikubwa kwa ustawi na uhai wa lugha za asili na lugha mama.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Mhadhiri Mwanndamizi, Dunlop Ochieng jana wakati akifunga mjadala wa kitaaluma kuhusu uhuishaji wa lugha mama uliofanyika katika Ukumbi wa chuo hicho, Kinondoni Jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wanataaluma wa ndani na nje ya nchi.

Alisema lugha mama na za asili zimetengwa na sera zilizopo kwa sasa licha ya kutanabaisha kuwa lugha hizo zina mchango mkubwa katika kuhifadhi utambulisho, historia, na hazina ya maarifa yasiyoonekana yanayoweza kurithishwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
“Sera zilizopo zinakandamiza lugha za asili kwa kuhimiza ujifunzaji wa lugha ya pili kwa gharama ya lugha ya kwanza (lugha ya mama),” alisema Dkt. Ochieng.
“Lugha kama Vidunda inayozungumzwa Mikumi, na Hadzabe inayozungumzwa katika mikoa ya Manyara na Singida zipo katika hatari kubwa ya kutoweka kutokana na athari za lugha zinazozungumzwa zaidi katika maeneo hayo,” alisema Dkt.Ochieng.
Alisema watoto wengi nchini wanakua bila kujifunza lugha za wazazi wao kutokana na kushamiri kwa Kiswahili pamoja na kasumba au mtazamo kuwa lugha za asili hazina umuhimu katika maisha ya kisasa.
“Lugha za asili hazipewi nafasi katika maeneo rasmi ya maamuzi na hutumika tu katika matukio ya kihistoria au sherehe maalum, lakini hazizingatiwi katika sera wala elimu,” alisema Dkt. Ochieng.
Mwanafunzi wa shahada ya Uzamivu katika Chuo Kikuu cha Warsaw nchini Poland, Talent Mudenda alitaja baadhi ya nchi ambazo zina sera na sheria zinazolinda lugha za asili licha ya kutokuwepo kwa kwa msukumo wa utekelezaji wake kutokana na kukosekana kwa tashi wa kisiasa.
“Nchi za Tanzania, Afrika ya Kusini na Zimbabwe zina sheria mahususi kwa ajili ya kulinda lugha za asili changamoto ni kusimamia utekelezaji wake”, alisema Mudenda.
Aidha alisema bado kunahitajika tafiti nyingi zaidi katika eneo la lugha mama na za asili ili kubaini matumizi na umuhimu wa lugha za hizo kwa jamii kulingana na miktadha ya uhtaji wake.
Darren Flavelle, Meneja wa Miradi ya Jamii kutoka Taasisi ya Maendeleo ya Lugha za Asili na Usomaji ya Watu wa Asili nchini Canada (CILLDI), Chuo Kikuu cha Alberta, alisisitiza umuhimu wa kuzilinda na kuzihuisha lugha za asili ulimwenguni ili kulinda upekee na utofauti wa kitamaduni na kujenga mifumo ya elimu jumuishi.
Kwa upande wake, Mhadhiri wa Lugha za Kigeni na Isimu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Ibrahimu Mussa alisema wakati mwingine watu huamua kutotumua lugha mama au za asili kwa makusudi fulani.
“Hatusomi tu lugha ili kuzijua bali tunaangalia faida zinazoambatana na lugha hizo”, alisema Dkt.Mussa.
Aidha alisema watanzania wengi wanatumia lugha za Kiwahili na Kiingereza kutokana na mahitaji yake kiofisi na katika seheemu rasmi.
Mjadala huo wa kitaaluma wa siku mbili uliandaliwa na kuratibiwa na Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii kwa kushirikiana na Idara ya Taaluma za Isimu na Fasihi pamoja na Kitengo cha Umataifishaji na Makongamano ya Kitaaluma na kuhudhuriwa na wataalamu wa lugha kutoka vyuo vikuu vya Tanzania, Burundi, Zimbabwe na Canada.
Leave a comment