Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase.

Na Gabriel Msumeno, Pwani

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Salim Morcase amekutana na wamiliki wa viwanda wa Mkoa huo ili kusikiliza changamoto mbalimbali zinazowakabili na kujadiliana nao namna bora za kuzitatua ili wafanye shughuli zao za uwekezaji vyema.

Mkutano huo ulifanyika leo kwenye ukumbi wa Polisi Kibaha mjini ni sehemu ya jitihada za Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano na makundi mbalimbali katika jamii na mwendelezo wa vikao na wafugaji, wafanyabiashara, waganga wa tiba asili, watu wenye ulemavu, maafisa usafirishaji, wawekezaji na wajasiriamali.

Alisema jeshi hilo linaendeleza falsafa ya Polisi Jamii kwa kukutana na watu wa makundi mbalimbali ili kuendelea kuimarisha mahusiano mema yatakayosaidia katika ulinzi na usalama kwa kuondoa matukio ya uhalifu.

Wamiliki wa viwanda walielezea changamoto zao za kiusalama, ikiwemo maeneo ya viwanda kuzungukwa na mapori, ubovu wa miundombinu ya barabara, na ukosefu wa vituo vya Polisi vya karibu, hali inayochangia kuongezeka kwa uhalifu hususani nyakati za jioni na usiku.

Baadhi ya wawakilishi viwanda mbalimbali Mkoani Pwani

Mwakilishi wa Wamiliki wa Viwanda Mkoa wa Pwani, Habibu Juma Issa kutoka kiwanda cha Bagamoyo Sugar alilishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani kufanya mkutano nao kwa lengo la kuimarisha ulinzi na usalama katika maeneo yote ya uwekezaji na kusaidia kukuza uchumi wa nchi kwa kujenga mazingira wezeshi kwa wawekezaji.

“Hii ni muhimu kwa kuwa itasaidia kuongeza ajira kwa vijana na kuongeza kipato, kuboresha doria na ulinzi maeneo ya viwanda ili tuweze kufanya kazi saa 24 kwa kupokezana usiku na mchana pasipo hofu ya kufanyiwa uhalifu na vibaka”, alisema Habibu.

Aidha, wamilki hao wa viwanda waliomba Jeshi la Polisi kutoa elimu kwa wawekezaji wageni kuhusu sheria na maadili ya kitanzania katika kazi ili kuepusha udhalilishaji na ukatili mahali pa kazi.

Akijibu baadhi ya hoja za washiriki katika mkutano huo, Kamanda Morcase alisisitiza kuwa kikao hicho ni fursa muhimu kwa Jeshi la Polisi kusikiliza changamoto zinazowakabili na kutafuta suluhu kwa pamoja na kuhaidi kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto zinazowezekana kutatuliwa mara moja.

Kwa changamaoto zilizopo ndani ya uwezo wetu tutazishughulikia lakini ambazo zitahitaji kushirikiana na na idara tutafanyia kazi baada ya kushirikisha mamlaka husika, alisema Kamanda Morcase.

Mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mkoa ya uwekezaji wenye takribani jumla ya viwanda 1,533 ambapo 33 kati yake ni viwanda vikubwa.

Posted in

Leave a comment