
Na Cartace Ngajiro
Umoja wa Wanawake Wanaofanya kazi Sekta ya Bahari Mashariki na Kusini mwa Afrika (WOMESA) wametembelea Bandari ya Tanga na kuridhishwa na utendaji kazi katika bandari hiyo baada ya kukamilika kwa mradi wa maboresho ya bandari.
Akiongea wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Umoja huo Mhandisi Fortunata Makoye Kakwaya alisema maboresho hayo yameleta mapinduzi makubwa katika bandari hiyo ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo meli kubwa zilikuwa haziwezi kufunga gatini kutokana na changamoto ya kina cha maji kuwa kifupi.

“Kama wadau katika sekta ya bahari tunapongeza kwa maboresho haya kwa kuwa yameleta mapinduzi makubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na kuifanya bandari hii ikidhi viwango vya kimataifa katika kuhudumia meli na mizigo”, alisema Mhandisi Kakwaya.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Bandari, Afisa Mkuu anayeshughulikia utekelezaji Gwakisa Mwaibuji aliwataka wadau hao kuwa mabalozi wazuri wa Bandari ya Tanga ili bandari hiyo iendelee kupokea shehena kubwa zaidi na mapato makubwa.


Leave a comment