
Na Gloria Maganza, Dodoma
Madereva wa magari ya serikali mkaoni Dodoma wametakiwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa kwa ajili ya usalama barabarani wanapokuwa wakiendesha magari hayo.
Rai hiyo imetolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Katabazi wakati akizungumza na madereva hao kwenye kikao maalumu alichokiitisha katika ukumbi wa Polisi jamii Jijini Dodoma kilicholenga kuzungumza nao juu ya utii wa sheria za usalama barabarani kwani baadhi yao wamekuwa wakilalamikiwa kukiuka sheria hizo.
“Kikubwa ni kuwataka madereva wa serikali kuzingatia sheria na taratibu zinazohusiana na usalama barabarani”, alisema Kamanda Katabazi.
Alisema Jeshi lake limekusudia kuwakumbusha na kuwaelimisha kuhussu sheria hizo, taratibu na kanuni lakini pia kuwaonya baadhi yao ambao hawazingatii sheria hizo kwa makusudi hivyo kuhatarisha usalama wao na wengine.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Madereva wa Serikali, Issa Kisebengo alisema elimu waliyoipata kwenye kikao hicho imewasaidia kutambua majukumu na wajibu wao kwenye utumishi wa umma na kutoa wito kwa madereva wenzake kuzingatia yale yote waliyofundishwa.

“Sisi ni vioo kwa madereva wengine lakini pia tunabeba watumishi wa serikali na kuna watumiaji wengine wa barabara na wote hao wanatutegemea sisi kwa usalama wao hivyo, mafunzo tuliyoyapata tutaenda kuyafanyia kazi”, alisema Kisebengo.
Sanjali na kukumbushwa sheria, kanuni na taratibu za usalama barabarani kikao hicho pia kiliambatana na mafunzo mbalimbali yaliyotolewa kwa madereva hao ili kuendelea kuwakumbusha sharia hizo kwani kuwa madereva wa magari ya serikali si kigezo cha kuvunja sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

Leave a comment