Na Vincent Mpepo

Wanataaluma na watafiti katika taasisi za elimu ya juu barani Afrika wametakiwa kufanya tafiti zitakazotoa majawabu ya matumizi endelevu ya rasilimali za bahari barani humo ili kutekeleza  dhana ya uchumi wa bluu kwa vitendo na tija katika kuchochea uchumi na maendeleo ya Afrika.

Wito huo umetolewa na washiriki katika mjadala wa kitaaluma uliofanyika leo katika ukumbi wa Hotel ya Johari Rotana, jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wasomi, wanataaluma viongozi wa serikali, taasisi binafsi na wanadiplomasia wa ndani na nje ya Afrika.

Akizungumza wakati akichangia mada mbalimbali zilizowasilishwa katika mjadala huo, Rais Mstaafu na Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA), Dr. Thabo Mbeki alisema bado kuna changamoto ya kueleweka kwa dhana ya uchumi wa bluu kivitendo.

“Asilimia kubwa ya watu wetu bado hawana maarifa sahihi kuhusu uchumi wa bluu na kwamba hatuna budi kuwaelimisha ili uchumi wa bluu ufahamike”, alsiema Rais Mstaafu Mbeki.

Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt.Dunlop Ochieng alisema kutokana na mjadala huo mojawapo ya vitu vya msingi ambavyo utekelezaji wa aina yoyote ya maendeleo unapaswa kuzingatia ni kuwaangalia wananchi wa kawaida watafaidikaje.

“Tunawekaje mazingira ya usalama wao kwani tumeona mara kadhaa utekelezaji wa shughuli za kiuchumi ikiwemo uwekezaji wananchi wamekuwa ni walaji wa mabaki na vinono vikisafirishwa kwenda nje”, alisema Dkt.Ochieng.

Alisema tunafamu umuhimu wa Mto Nille kwa nchi ya Misri na kwamba dhana ya uchumi wa bluu wakati mwingine ni msamiati tu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku alisema Afrika inahitaji vinara watakaofanya kazi mstari wa mbele ili kuhakikisha malengo ya kujikomboa kifikra na kujiamini yanatimia.

“OAU imesaidia nchi za Afrika kupata Uhuru wake lakini kwa sasa AU na Afrika ya sasa ni kulikomboa Bara hilo katika nyanya zote za kiuchumi, kisiasa na kijamii”, alisema Butiku.

Aidha alimshukuru Rais Thabo Mbeki kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mjadala huo uliosaidia kufanya tathimini ya thamani ya uchumi wa bluu katika bara la Afrika na kuanisha mikakati ya kutumia rasilimali za bahari kujikomboa kiuchumi.

Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi wa masuala ya rasilimali za bahari, Dkt. Narriman Jiddawi alielezea mabadiliko ya kiutamaduni na kifikra yanayoonesha kukua kwa ushiriki wa wanawake wa Zanzibar kwenye uchumi wa bluu na kwamba wanajihusisha na shughuli mbalimbali za kujipatia kipato zinazoambatana na rasilimali za bahari.

Posted in

Leave a comment