
Na Gloria Maganza, Dodoma
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kondoa pamoja na wananchi wa Kata ya Haubi wamefanikisha operesheni maalumu ya kutokomeza kilimo haramu cha bangi katika maeneo ya Hifadhi ya Milima ya Haubi, wilayani Kondoa, mkoani Dodoma.
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa DCEA, Naibu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali wa Mamlaka hiyo, Daniel Kasokola, alisema operesheni hiyo iliyofanyika kuanzia Mwezi Mei 14 hadi 19,2025 na imefanikisha kuteketeza ekari 157 za mashamba ya bangi yaliyokuwa katika vijiji vya Ntomoko, Kinyasi na Haubi.
Aidha, watuhumiwa saba wanashikiliwa kwa mahojiano huku pikipiki mbili zikikamatwa katika maeneo ya operesheni.
“Operesheni hii ni ya pili kufanyika mwaka huu katika wilaya ya Kondoa ambapo mwezi Januari tulibaini na kuteketeza zaidi ya ekari 500 za bangi”, alisema Kasokola.
Alisema kupungua kwa mashamba hayo kutoka ekari 500 hadi 157 ni ushahidi kuwa wananchi wameanza kuelewa na kushiriki kikamilifu katika jitihada hizi na kwamba anapongeza kwa ushirikiano wao unaowezesha operesheni hiyo kufanikiwa.

Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Fatuma Nyangasa amesisitiza kuwa serikali ya Wilaya ya Kondoa itaendelea kushirikiana kwa karibu na mamlaka hiyo kuhakikisha kilimo cha bangi kinatokomezwa kabisa na kusisitiza kuwa elimu kwa wananchi itaendelea kutolewa ili waachane na kilimo haramu badala yake wajikite katika uzalishaji wa mazao halali ya chakula na biashara kama vile tumbaku, ufuta na maharage.
“Serikali ipo tayari kuwaongoza katika kilimo halali na chenye tija badala ya bangi, zaidi niwaombe wanachi washirikiane naserikali”, alisema Nyangasa.
Aidha Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya itaendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayejihusisha na kilimo, biashara au usambazaji wa bangi na dawa nyingine za kulevya.

Leave a comment