
Meneja wa Mamlaka Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa akielezea majukumu mbalimbali ya Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa madereva wanaosafirisha kemikali kutoka kampuni ya Golden Coach jijini Dar es Salaam.
Na Okello Thomas
Madereva wanaosafirisha kemikali hatarishi wametahadharishwa kutotumia dawa za kulevya wanaposafirisha kemikali hatarishi ili kujiepusha na ajali za barabarani zinazochangiwa na madhara ya dawa hizo.
Tahadhari hiyo imetolewa leo na Meneja wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali Ofisi ya Kanda ya Mashariki, Danstan Mkapa wakati akifunga mafunzo kwa madereva wanaosafirisha kemikali kutoka kampuni ya Golden Coach ya Dar es Salaam hivi karibuni katika ukumbi wa mafunzo wa Golden Coach.
“Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali imeona umuhimu wa kuandaa mafunzo haya kwa madereva wanaosafirisha kemikali hatarishi kwa kuwa wengi ni vijana na nguvu kazi ya taifa”, alisema Mkapa.
Alisema madereva wote wanaosafirisha kemikali hatarishi wanapaswa kuepuka kuendesha vyombo vya moto wakiwa wametumia vilevi kwasababu ni hatari kwao na ukizingatia mzigo wanaobeba na mazingira wanayopita na kuhitaji umakini sana.
Aidha, alisema matumizi ya madawa ya kulevya wakati wa usafirishaji, huathiri uwezo wa kufikiri, kutafakari na uwezo wa kuona jambo ambalo dereva anageweza kulifanyia maamuzi sahihi ili kuwa na thadahari za haraka bila kusabisha ajali ajali ambazo zingeweza kuzuilika.
Mkapa ametoa rai kwa wamiliki wa kampuni za kusafirisha kemikali hatarishi kuendelea kutoa elimu kwa madereva wao kuhusu ufahamu wa makundi ya kemikali wanazosafirisha kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini.
Dereva wa kampuni ya Golden Coach, Saidi Kisindula alisema baada ya kupata mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali kutoka Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali itawasaidia kuwa makini katika kazi hiyo.

Madereva kutoka kampuni ya Golden Coach wakifuatilia mafunzo ya usafirishaji salama wa kemikali yaliyotolewa na Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Alisema wataendelea kuwa mabalozi kwa kuendelea kutoa elimu hiyo kwa madereva wenzao wanaofanya kazi hiyo ya usafirishaji wa kemikali katika makampuni mbambali nchini.
Leave a comment