Na Vincent Mpepo

Nchi za Afrika zimetakiwa kuunganisha nguvu na kufanya kazi kwa kushirikiana badala ya kila nchi peke yake ili kupiga vita umaskini na kujikwamua dhidi ya unyonyaji na kuenzi ndoto na maono ya waasisi wa bara la Afrika ikiwemo Mwalimu Julius Nyerere na Neslon Mandela.
Hayo yalibainishwa na washiriki wa mjadala wa kitaaluma uliofanyika hivi karibuni katika ukumbi wa Hotel ya Johari Rotana, jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wasomi, wanataaluma viongozi wa serikali, taasisi binafsi na wanadiplomasia wa ndani na nje ya Afrika.
Akiwasilisha mada katika mjadala huo, Profesa Senia Nhamo kutoka Chuo Kikuu cha Afrika Kusini (UNISA) alisema bado kuna faida kuwa ya kuungana na kufanya kazi pamoja kutokana na fursa za kiuchumi zinazopatikana kati ya mataifa ya Afrika ambayo inaweza kuwapa nguvu ya kiuchumi.

“Tunaweza kutumia rasilimali zetu na kufanya biashara kati yetu ikiwa tutapunguza urasimu na vikwazo katika kodi na ushuru wa forodha”, alisema Profesa Nhamo.
Alibainisha baadhi ya changamoto ambazo zikifanyiwa kazi zinaweza kusaidia katika kuboresha uchumi wa Afrika ikiwemo matumizi ya fedha moja pamoja na kundoa vikwazo vya ushuru wa forodha.
Aidha alizitaka serikali barani Afrika kuwekeza kwenye tafiti zenye tija na kwamba taasisi za elimu ya juu zisifungie tafiti kwenye maktaba badala yake matokeo ya tafiti yawe wazi kwa wananchi na yasaidie utatuzi wa chngamoto za jamii husika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Julius Nyerere, Joseph Butiku alisema Afrika inahitaji kuwa na mwendelezo wa mipango endelevu kiuongozi ili kufikia maendeleo inayoyakusudia.

“Kuna shida ya kutokuwepo kwa mwendelezo wa mipango na utekelezaji wa vipaumbele vya kimaendeleo kutokana na mabadiliko ya uongozi hivyo kuendelea kubaki nyuma”, alisema Butiku.
Alisema kila wakati na kila uongozi huja na vipaumbele vyake vya kiutekelezaji ambavyo wakati mwingine huwa ni vipya badala ya kuendeleza walivyovikuta ambavyo vilianzishwa na watangulizi wao.
Aidha alimshukuru Rais Thabo Mbeki kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa mjadala huo uliosaidia kufanya tathimini ya thamani ya uchumi wa bluu na kwamba uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini ni wa kihistoria tangu nyakati harakati za kupigania Uhuru.
Kwa upande wake, Mtafiti kutoka Chuo cha Taifa cha Ulinzi-Tanznia, Dkt. Lucy Shule alisema ushirikiano kati ya nchi na nchi na kikanda barani Afrika ni mojawapo ya mikakati itakayosaidia kuivusha Afrika kiuchumi kwa kuwa ushirikiano huongeza nguvu katika kufanya jambo badala ya kila nchi kufanya peke yake.
Aidha akizungumzia uchumi wa blue endelevu alisema bado kuna haja ya serikali za nchi za Afrika kutoa elimu ya dhana ya uchumi wa bluu na kuweka sera za ulinzi kwa wazawa ili wawe wanufaika wa mazao yanayotokana na rasilimali za bahari.
Mkuu wa Kitivo cha Sanaa na Sayansi za Jamii wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Dkt.Dunlop Ochieng alisema wakati mwingine mipango inayohusisha maendeleo ikiwemo uwekezaji imekuwa ikiwabagua wenyeji na matokeo yake ni kutopata ushirikiano mzuri.

Alisema katika kila aina ya shughuli ya maendeleo inayopaswa kufanyika mahali popote ni muhimu kuzingatia wazawa ili wawe ni sehemu ya maendeleo hayo badala ya kuwa wasindikizaji kwenye ardhi yao.
Leave a comment