
Na Vincent Mpepo
Mwinjilisti Neema Mhilu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema suala la wakristo kuishi pamoja ni suala la kibiblia na kusisitiza kuwa Umoja wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania unasawiri uhalisia huo.
Mwinjilisti Mhilu aliyasema hayo jana wakati wa mahuburi katika ibada ya Siku ya 5 baada ya Pasaka katika Mtaa wa Kwembe ambapo kwa mujibu wa kalenda ya KKKT ni siku ya Umoja wa Jumuiya ya Kikristu Tanzania yaani (CCT).
Alisema biblia inaagiza ndugu wakae pamoja kwa upendo akirejelea maneno kutoka kitabu cha Warumi 12:13-15 na kwamba kuishi pamoja kuna faida nyingi ikiwemo namna bora ya kujaliana na kuhudumiana tukiwa hapa duniani.
“Suala la umoja ni suala la kibiblia na lilianzishwa na Yesu mwenyewe”, alisema Mwinjilisti Mhilu
Alisema wakristo wanapaswa kuuenzi umoja huo kwa sababu kufanya hivyo ni kutekeleza maagizo ya Mungu na upendo ukitawala kuna faida nyingi ikiwemo kuishi kwa mshikamano na amani katika ngazi ya mtu na mtu lakini pia hata katika jamii na taifa na kuhusiana vyema na watu wengine wasio wakristo.
“Umoja huu ulinzishwa Mwaka 1934 na una vyama na taasisi 24 kwa madhumuni ya kumhubiri kristo ndani na nje ya Tanzania”, alisema Mwinjilisti Mhilu.
Aidha aliwataka wakristo kuuishi ukristo wao kwa matendo kwa kuwa matendo mema yanaendana na nguvu itakayowatambulisha kwa watu wasio wakristo ambao wanatambua nguvu na thamani ya ukristo na kuwaasa kubaki katika Imani zao badala ya kuhamahama kufuata miujiza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Ujenzi Mtaani hapo, Exaud Mchome aliwataarifu washarika kuhusu kukamilika kwa kazi ya kuezeka jengo la kanisa na ambalo linaendelea kujengwa kwa sadaka za washarika mtaani hapo.

“Sehemu zilizobaki zitafanyiwa kazi kwa ushauri wa Mchungaji na katika kikao chetu cha leo tutafanya maamuzi ili kufikia wiki ijayo kazi hiyo iwe imekamilika kabisa”, alisema Mzee Mchome ambaye kwa sasa anafahamika kwa jina la Hagai.
Aliwakumbusha washarika kuendelea kukamilisha ahadi zao kwa awamu ya kwanza iliyoanza Januari mpaka Juni Mwaka 2025 huku akiwahakikishia kuwa taarifa ya mapato na matumizi ya pesa hizo zitaletwa kwa washarika ili waone.

Mtendakazi wa Mtaa huo, Anna Mauki aliwakumbusha washarika mambo kadhaa ikiwemo kuhudhuria ibada ya siku ya kupaa kwa Bwana itakayofanyika siku ya Alhamisi na kuendelea kutoa sadaka ya ujenzi wa kituo cha kimataifa cha watoto wenye mahitaji maalumu ambacho kinahamishwa kutoka Kijichi kwenda Dar es salaam Kitopeni, Bagamoyo.
Leave a comment