
Na Gloria Maganza, Dodoma
Serikali imetangaza utekelezaji wa Mkakati wa Kitaifa wa Matumizi ya Teknolojia za Kidijitali katika elimu ikijumuisha miongozo ya matumizi ya teknolojia katika shule, Vyuo vya Ualimu, Vyuo vya Ufundi na Vyuo Vikuu, pamoja na matumizi ya akili bandia (Artificial Intelligence) kwa mwaka 2025.
Kauli ya utekelezaji mkakati huo ilitolewa jana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo Jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya serikali ya wamu ya sita na kubainisha maeneo kadhaa ya maboresho yatakayoongeza tija katika sekta ya elimu.
Alisema katika sekta ya elimu ya juu serikali imeanza ujenzi wa majengo ya madarasa, maabara na mabweni katika kampasi kuu na za pembezoni katika mikoa 16 ambayo haikuwa na taasisi za elimu ya juu.
Ujenzi huo unatokana na Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) wenye thamani ya shilingi bilioni 972 na utaongeza uwezo wa taasisi za elimu ya juu nchini kudahili wanafunzi zaidi na kupunguza uhaba wa wahadhiri kwa asilimia 20.
“Tunahakikisha kwamba elimu yetu inazalisha wataalamu wenye ujuzi na stadi zinazohitajiwa katika soko la ajira ili kuchangia maendeleo ya Taifa letu,” alisema Profesa Mkenda.
Alisema pamoja na mafanikio hayo serikali imeandaa Mfumo wa Kielektroniki wa Tathmini ya Ujifunzaji unaolenga kurahisisha upimaji wa wanafunzi katika shule za msingi na kuimarisha huduma kwa walimu na wanafunzi wenye mahitaji Maalumu na maboresho ya mitaala katika ngazi zote za elimu.
“Serikali inaendelea kuimarisha mfumo wa elimu kupitia maboresho makubwa ya mitaala katika ngazi zote za elimu nchini ili kuongeza ujuzi, maarifa, tina na stadi za wanafunzi wanaohitimu”, alisema Profesa Mkenda.
Alisema serikali imeweka mfumo wa elimu nyumbufu ili kuhakikisha wanafunzi wanapokea ujuzi na maarifa yanayozingatia mahitaji halisi ya taifa na soko la ajira.
“Tumeweka somo la lazima la elimu ya biashara na historia ya Tanzania huku tukiboresha mifumo ya ufundishaji lugha ili kuongeza ufanisi wa ujifunzaji,” alisema Profesa Mkenda.
Alisema mitaala 389 katika elimu ya ufundi na mitaala 563 katika elimu ya juu imeboreshwa ili kuendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014, Toleo la 2023 pamoja na kuzingatia stadi za karne ya ishirini na mahitaji ya kitaifa, Kikanda na Kimataifa.
“Serikali inaendelea kufanya mapitio ya Sheria ya Elimu (Sura 353) ili kuendana na mabadiliko haya ya sera na mitaala”, alisema Profesa Mkenda.
Alisema wizara yake inaendelea kukusanya maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu ili kuhakikisha sheria husika inakidhi mahitaji ya sasa ikiwemo ushirikishwaji wa umma.
Aliongeza kuwa serikali imehuisha miongozo mbalimbali ikiwemo Mwongozo wa Taifa wa Tuzo na Sifa Linganifu za Kitaaluma (TQF), Mwongozo wa Uanzishaji na Usajili wa Shule, Mwongozo wa Utambuzi wa Vipawa na Vipaji, pamoja na Mwongozo wa Mafunzo Endelevu ya Walimu Kazini.
Aidha, Waziri Mkenda amewataka wananchi na wadau wa elimu kuendelea kushirikiana na serikali katika kuimarisha mfumo wa elimu nchini ili kuhakikisha elimu inakuwa chachu ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.

Leave a comment