

Na Gloria Maganza, Dodoma
Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Meja Jenerali Rajabu Mabele ametoa wito kwa vijana wote waliohitimu kidato cha sita mwaka 2025 kutoka shule zote Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa mujibu wa sheria kwa mwaka 2025.
Akiwasilisha wito huo jana kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Kijenga Taifa JKT Jijini Dodoma, Kaimu Mkuu wa Utawala wa JKT, Kanali Juma Mrai amesema vijana hao wanatakiwa kuripoti kwenye kambi mbalimbali kuanzia Mei 28 hadi Juni 08, 2025.
Alitaja kambi ambazo wahitimu hao watakwenda kuripoti kuwa ni JKT Rwamkoma – Mara, JKT Msange – Tabora, JKT Ruvu na JKT Kibiti – Pwani, JKT Mpwapwa na JKT Makutupora – Dodoma, JKT Mafinga -Iringa, JKT Mlale – Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba -Tanga, JKT Makuyuni na JKT Orjolo – Arusha.
‘Kambi nyingine ni JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila – Kigoma, JKT Itaka – Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa – Rukwa pamoja na JKT Nachingwea – Lindi”, alisema Kanali Mlai.
Alisema wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho (Physical Disabilities) watatakiwa kuripoti katika Kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa aina hiyo.
Aidha aliwahimiza wazazi na walezi kuwapa ruhusa vijana wao kuhudhuria mafunzo hayo muhimu kwa maendeleo na kwa maisha yao ya baadae.
Mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria yanalenga kuwajenga vijana katika ujasiri, nidhamu na kuimarisha maadili ya kizalendo.
Leave a comment