Wadau wa Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu katika picha ya pamoja leo wakati wa warsha ya mapitio ya Mtaala wa Shahada ya Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu iliyifanyika leo jijini Dar es salaam na kuhusisha wanataaluma, waanafunzi, wahitimu, waajiri, vyama vya kitaaluma na wafanyakazi katika kada hiyo katika sekta za umma na binafsi.

Na Vincent Mpepo

Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) kitaanza kutoa programu ya Shahada ya Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu kuanzia mwaka wa masomo wa 2025/2026 baada ya kutimiza vigezo na masharti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU).

Akizungumza wakati wa warsha ya wadau kuhusu programu hiyo leo Kinondoni, jijini Dar es salaam, Mhadhiri Msaidizi wa chuo hicho, Chausiku Mwinyimbegu alisema programu hiyo imelenga kutoa mafunzo kwa watu wenye msingi na wasio na msingi wa kitaaluma katika fani za utunzanji wa nyaraka, kumbukumbu, ukutubi na masomo ya taarifa ambao wana nia ya kufuata taaluma hiyo.

“Lengo la programu hii ni kutoa mafunzo bora na kufundisha wataalamu wa usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu,” alisema Mwinyimbegu.

Alisema programu hiyo itafundishwa kupitia mfumo wa elimu huria na masafa na kwamba chuo kinatarajia kudahili wanafunzi wanaotamani kujijenga kitaaluma katika eneo hilo.

Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam (DarTU), Dkt. Getrude Ntulo alisema wamepitia programu hiyo kwa kina katika maeneo mbalimbali ikiwemo jina, maudhui, uhalisia wa programu na namna ilivyozingatia vigezo na masharti ya Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania.

“Masuala mengine yaliyoshughulikiwa ni pamoja na kuhakikisha programu hiyo inaendana na Sera ya Elimu na Mafunzo ya sasa pamoja na mahitaji ya mapitio ya mitaala kama yanavyoelekezwa na wizara inayohusika ambayo yanasisitiza elimu inayozingatia umahiri”, alisema Dkt. Ntulo.

Aidha aliipongeza Idara ya Masomo ya Habari na Ukutubi chuoni hapo kwa kazi nzuri waliyofanya katika uandaaji mtaala wa programu hiyo kwani anatambua siyo kitu rahisi kwa kuwa kinahusisha juhudi na kujitoa.

Kwa upande wake, Mhadhiri Mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dkt. Esther Ndenje alisema wamependekeza mpangilio mpya wa wa mada mbalimbali ili kuhakikisha mpangilio wa kufundishia unafuata mtiririko wa mantiki na uelekevu wa kitaaluma.

“Mara nyingine ni rahisi kuweka mada ndogo kwenye mtaala lakini changamoto hujitokeza wakati wa kufundisha darasani,” alisema Dkt. Ndenje.

Mwanafunzi wa Shahada ya Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC), Martha Mohamed, alisema ni muhimu kwa taasisi za elimu ya juu kuwashirikisha wadau katika mchakato wa kuanzisha programu mpya ili kupata maoni kuhusu maudhui ya programu ili kuoata kuunda mtaala bora.

“Kuwashirikisha wadau mbalimbali wa taaluma husika kutasaidia vyuo na taasisi za elimu ya juu kupata maudhui bora katika usimamizi wa nyaraka na kumbukumbu,” alisema Martha.

Mhadhiri Msaidizi na Mratibu wa programu hiyo, Ntimi Kasumo aliwashukuru wadau wa ndani na nje walioudhuria kwa michango yao ambayo itasaidia kuboresha mtaala wa programu hiyo ili kupata wahitimu watakaokidhi vigezo na kukubalika katika soko la ajira ambalo msingi wake ni umahiri.

Wadau wa Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu katika picha za Makundi namba  1, 2 na 3 wakati wa mijadala iliyofanyika leo wakati wa warsha ya mapitio ya Mtaala wa Shahada ya Utunzaji wa Nyaraka na Kumbukumbu jijini Dar es salaam ikihusisha wanataaluma, waanafunzi, wahitimu, waajiri, vyama vya kitaaluma na wafanyakazi katika kada hiyo katika sekta za umma na binafsi.

Posted in

Leave a comment