Issa Mwandagala, Songwe

Madereva wanaosafirisha abiria na mizigo kwenda sehemu mbalimbali ndani na nje ya Mkoa wa Songwe wametakiwa kufuata sheria za usalama barabarani ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za madereva wenzao wazembe ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Charles Bukombe baada ya kufanya oparesheni ya ukaguzi wa magari ya abiria na mizigo katika Kituo cha Ukaguzi wa Magari Mkoani humo eneo la Chimbuya Wilaya ya Mbozi.

SSP Bukombe alisema lengo la operesheni hiyo pamoja na ukaguzi huo ni kuangalia ubovu wa magari hasa ukaguzi wa mataili, kukagua madeni ya magari ambayo bado hayajalipwa, ukaguzi wa leseni, ujazaji wa abria kupita uwezo wa chombo pamoja na ukaguzi wa tiketi mtandao ili kuepusha ajali zinazoweza.

“Niwaombe madereva na abiria kutofumbia macho vitendo vya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani na badala yake mnatakiwa kukemea na kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili hatua za haraka zichukuliwe” alisema SSP Bukombe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Wilaya ya Mbozi Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Anton Sabasaba alisema jeshi la polisi linaendelea kutoa elimu kwa abiria juu ya umuhimu wa kufichua taarifa za madereva wazembe wasiofuata sheria za usalama barabarani.

Alisema Jeshi la Polisi nchini linaendelea na operesheni za ukaguzi wa vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na utoaji elimu kwa jamii kuhusu masuala ya usalama barabarani ili kutokomeza ajali za barabarani kwa watumiaji wa vyombo vya moto na watembea kwa miguu na kupunguza ajali ambazo zinaepukika.

Katika operesheni hiyo jumla ya magari 54 yalikaguliwa na kati ya hayo magari 8 yalikutwa na changamoto ambazo zinaweza kusababisha ajali ikiwa ni pamoja na kasoro katika leseni 17 za madereva.

Posted in

Leave a comment