

Na Stella Ngenje-Mlete
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Shirika la Umeme Tanzania -Tanesco Mkoani Ruvuma imeanza kulipa fidia kwa wananchi waliopisha maeneo yao kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa gridi ya taifa ya Msongo wa 220KV kutoka Songea hadi Tunduru ambapo zaidi ya wananchi 200 watanufaika na fidia hiyo.
Wanufaika wa fidia hiyo ni wale wanaoishi kijiji cha Mlete, Kata ya Shule ya Tanga Manispaa ya Songea na kwamba kukamilika kwa mradi huo kutachochea shughuli za kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja hivyo kukuza pato la taifa.
Akizungumza na wananci wa maeneo yaliyolipiwa fidia, Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja Tanesco Mkoa wa Ruvuma, Alan Njiro aliwataka wakazi wa maeneo hayo kutorejea tena ili kupisha utekelezaji wa mradi huo.
“Nishati ya umeme imewafikia wananchi wa Mlete hivyo ni jukumu la kila mmoja wenu kuwa mlinzi wa miundombinu hii ili kuendelea kunufaika nayo kwa muda mrefu”, alisema Njiro.
Aidha alisema serikali itaendelea kuboresha huduma ya umeme na kuwaasa wananchi hao kutoa taarifa kwa kupiga simu bure kupitia namba 180 kwa maulizo, dharura na uhitaji wa huduma nyingine.
Mtumishi wa Tanesco kutoka Makao Makuu, Phlasida Lalika aliwaasa wananchi kutumia vizuri fedha za fidia kwa kuanzisha miradi na shughuli za ujasiriamali ili kujiongezea kipato.
Mtumishi Mwingine wa Tanesco, Winifrida Masuka alisema wameenda kijijini hapo ili kuwahakikishia kuwa serikali kupitia Tanesco itawalipa fidia hizo kwa wakati ili watafute maeneo mbadala.
Kwa Upande wao wanufaika wa fidia hiyo wameishukuru Tanesco pamoja na Serikali kwa kuwa malipo hayo yamekuja wakati muafaka na kwamba pesa hiyo itasaidia katika shughuli mbalimbali ikiwemo kutafuta maeneo mbadala na kulipa ada za watoto.
Afisa Tarafa Songea Mjini Mashariki, Dismas Komba ni alishukuru serikali kwa kazi kubwa na nzuri ya kuwaletea maendeleo wananchi na kwamba mchakato wa uthaminishaji wa maeneo ya wananchi ulianza Mwezi Mei 2023.
“Ofisi yangu na ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Songea zinawashauri kutumia vyema pesa za fidia kwa ajili ya ujenzi wa makazi badala ya kufanya vitu visivyofaa ikiwemo kuoa wanawake”, alisema Komba.
Licha ya kuipongeza serikali kwa kusogeza huduma muhimu kwa wananchi alisema umeme utakaopatikana katika mradi huo utachochea kasi ya maenedeleo na kuvutia wawekezaji kupitia viwanda na shughuli nyingine zinazotegemea nishati ya umeme.

Maafisa wa Tanesco Kutoka Mkoa wa Ruvuma na waandishi wa habari walifika kijiji cha Mlete ilipo ofisi ya Mtaa ambako zoezi la kukabidhi hundi na kuwafungulia akaunti wananchi linaendelea huku kiasi cha shilingi bilioni 2.5 zinaendelea kulipwa kwa wananchi waliopisha maeneo yao kuruhusu mradi huo.

Leave a comment