Na Cartace Ngajiro, Tanga

Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Dadi  Kolimba amewapongeza watumishi wa Bandari ya Tanga na kuwataka waendelee kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono juhudi za serikali katika uwekezaji mkubwa uliofanyika katika bandari hiyo.

Kolimba alitoa pongezi hizo baada ya kutembelea na kukagua banda la Bandari ya Tanga kwenye  maonesho  ya 12 ya Biashara na Utalii  (Tanga Trade Fair) yanayofanyika katika viwanja vya Mwahako  kuanzia tarehe 28 Mei hadi 6 Juni 2025.

“Serikali imewekeza kiasi cha Shilingi za Kitanzania Billioni 429.1 hivyo endeleeni kuwajibika ipasavyo ili uwekezaji huo uweze kuzaa matunda sabamba na uhudumiaji wa shehena na ukusanyaji wa mapato uzidi kuongezeka” alisema Kolimba

Akitoa maelezo kwa  Mkuu wa Wilaya huyo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Usaidizi wa Biashara Bi. Rose Tandiko kwa niaba ya Meneja wa Bandari, alisema Bandari ya Tanga imeshiriki katika maonesho hayo kwa utoaji wa elimu kwa umma juu ya faida itakayopatikana baada ya mradi huo kukamilika.

Bi. Rose alitoa rai kwa wafanyabiashara kuitumia Bandari ya Tanga kwani huduma zake zimeboreshwa na hakuna msongamano kutokana na utendaji kazi wenye ufanisi na wafanyakazi wenye ari kubwa.

Alisema uwekezaji uliofanywa na serikali umekusudia kuijengea uwezo bandari hiyo ili iweze kuhudumia shehena kutoka tani 750,000 hadi tani 3,000,000 kwa mwaka.

Maonesho ya 12 ya Biashara na Utalii ambayo husimamiwa na Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) ambapo kauli mbiu mwaka huu ni  “Mwonekano wa Wadau Sekta ya Umma na Binafsi Kwenye Uwekezaji, Ukuaji na Uendelevu wa Biashara”.

Posted in

Leave a comment