
Na Vincent Mpepo, Dodoma
Washarika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) wamekumbushwa kuendelea kumtolea Mungu kwa hiari kwani matendo ya utoaji yana baraka na Mungu hupendezwa na wenye moyo wa shukrani.
Akihubiri wakati wa ibada ya kwanza jijini Dodoma katika Usharika wa Kanisa Kuu, Mchungaji Kiongozi wa KKKT Usharika wa Kisamo, Jimbo la Kaskazini Kati-Moshi, Theophilus Mghase alisema kumtumikia Mungu kwa njia ya utoaji, hiari na moyo wa kupenda ndio nguzo ambayo huwanufaisha wakristo kwa baraka kutoka kwake.
Alisema wakati usharika huo unazindua utoaji sadaka kwa minajiri ya ununuzi wa gari kwa ajili ya matumizi ya usharika ni vyema kila msharika akaona namna ambavyo anadhihirisha uwepo wake kwa kufanya jambo litakaloacha alama ili Mungu ambariki.
“Uwepo wako usababishe kitu cha Mungu kifanyike na utambue kuwa upo kwa kusudi lake”, alisema Mchungaji Mghase.
Alisema siri kubwa ya mafanikio ni kumtumikia Mungu kwa furaha na kumtolea kwa hiari bila manung’uniko yoyote.
Alibainisha faida za kumtumikia Mungu kuwa ni pamoja na kupata kibali katika masuala mbalimbali ya ikiwemo kazini na baraka katika maisha yetu akilejelea maandiko matakatifu kutoka Zaburi 100.
Aliongeza faida nyingine ya kumtumiia Mungu kwa njia ya matoleo ni kuwa na uhakika wa ulinzi katika mali zetu, kazi zetu na shuhguli mbalimbali za kujiingizia kipato.
“Unapoona biashara yako inanawiri mfano duka linaleta wateja ni kwa sababu ya kibali kilichoachiliwa na Mungu kwa ajili yako”, alisema Mchungaji Mghase.
Alisema mafanikio mengine ni pamoja na kupanda vyeo, kupata kazi na heshima katika nyumba zetu na jamii siyo kwa sababu ya umaarufu wao bali ni neema ya Mungu wanayotembea nayo na kwamba kumtegemea Mungu ni ulinzi dhidi ya roho za uharibifu katika mafanikio na maisha yao yao kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mchungaji Kiongozi wa Usharika huo, Daniel Sailowa alisema usharika wake unaendelea na utekelezaji wa malengo waliyojiwekea akibainisha ujenzi wa hoteli na sehemu ya kanisa.
“Malengo mengine ni kununua gari kwa ajili ya matumizi ya usharika ikiwemo kazi ya injili”, alisema Mchungaji Sailowa.
Alisema gari hilo litasaidia katika uinjilishaji vijijini na kuwa na chombo cha usafiri chenye hadhi na kwamba gari lililopo limesaidia kwa muda na limechoka.
“Tunakusudia kununua gari lenye thamani ya shilingi 120 na mpaka sasa tayari tuna shilingi milioni 65 na tunahitaji nguvu ya pamoja kukamilisha hiyo milioni 55 iliyobaki ili kufikia malengo mwaka huu”, alisema Mchungaji Sailowa.

Leave a comment