
Na Gabriel Msumeno, Pwani
Timu ya madaktari bingwa chini ya mpango maalum wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan imewasili mkoani Pwani kwa ajili ya kutoa huduma za kibingwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.
Mratibu wa timu hiyo kutoka Wizara ya Afya, Joachim Masunga amesema ujio wa madaktari hao kwa mara ya tatu mkoani humo unalenga kupunguza changamoto zinazowakabili wakazi wa Pwani ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilazimika kusafiri umbali mrefu hadi Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kupata huduma za kibingwa.
“Ujio wa madaktari hawa unalenga kupunguza gharama na usumbufu wa usafiri wa wagonjwa pamoja na kuimarisha huduma za afya katika mkoa huu,” alisema Masunga.

Alisema madaktari hao watakuwa mkoani Pwani kwa kipindi cha siku tano na wamesambazwa katika hospitali za halmashauri zote tisa za mkoa huo ili kuhakikisha huduma zinawafikia wananchi kwa usawa na kwa wakati.
Akizungumza baada ya kuwapokea madaktari hao, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Dkt. Kusirie Ukio alisema ujio wa timu hiyo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma za afya na kupunguza idadi ya rufaa zinazotumwa Muhimbili.
“Ujio wa madaktari hawa utasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza rufaa hizo na kuleta unafuu kwa wagonjwa na familia zao,” alisema Dkt. Ukio.
Mpango huu ni sehemu ya jitihada za serikali kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana hadi ngazi za chini na kwamba kila mtanzania anapata huduma stahiki bila vikwazo vya kijiografia au kiuchumi.

Leave a comment