Na Issa Mwandagala

Wazazi na walezi Mkoani Songwe wametakiwa kutoruhusu watoto wenye jinsi tofauti kulala katika chumba kimoja kwani ndio chanzo cha mmonyoko wa maadili kwani wengi huanza kujihusisha na mahusiano ya kimapenzi katika umri mdogo.

Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Akama Shaaban wakati akitoa elimu ya madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wazazi, walezi na watoto waliofika   kwa ajili ya michezo mbalimbali katika Kituo cha kutambua na kukuza vipaji vya watoto kiitwacho Mwakitwange Toto Center kilichopo maeneo ya Isangu Wilaya ya Mbozi.

Alisema uzoefu na tafiti zinaonesha kuwa vitendo vya watoto kujiingiza katika mahusiano ya kimapenzi vinaanzia majumbani ambapo watoto wenye jinsi mbili tofauti wanalala chumba kimoja.

Sanjali na hilo alisema wazazi na walezi wanapaswa kuwa makini na wageni, ndugu au jamaa wanaowatembelea na kutorusu wageni hao kulala na watoto wao kwani wakati mwingine ndio chanzo cha mahusiano wakiwa wadogo na kuhatarisha mfumo wao wa akili.

Alisema watoto wanapoanza vitendo vya mahusiano ya kimapenzi katika umri wadogo ni sababu ya kutokuwa na mwamko wa kimasomo na badala yake hujiingiza kwenye vitendo hivyo na watu wenye umri mkubwa ambapo ndio chanzo cha ukatili wa kijinsia.

“Kuwalaza chumba kimoja ndugu, jamaa au marafiki wanaowatembelea na watoto wetu ni ukatili kwa watoto”, alisema ACP Akama.

Kwa upande wake Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Songwe, Mkaguzi wa Polisi Eletisia Mtweve amewataka wanaume kutotelekeza watoto wao kwani kufanya hivyo ni chanzo cha kuwa na watoto wa mitaani na ongezeko la waanaofanyiwa vitendo vya ukatili ikiwemo kubakwa na kulawitiwa.

Koplo Gladness Sizya alisema ni jukumu la kila mzazi/mlezi kuhakikisha anatoa huduma bora kwa mtegemezi wake ili kupunguza vitendo vya ukatili na unyanyasaji dhidi ya watoto katika jamii ili kuwa na mazingira rafiki na salama yatakayowasaidia kutimiza ndoto zao.

Mkurugenzi wa kituo hicho Bi. Rita Kamenya amelishukuru kwa dhati Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kwa kushiriki katika tukio hilo na alitumia fursa hiyo kubainisha huduma zitolewazo kituoni hapo na hakusita kuelezea furaha yake kwa elimu iliyotolewa na kuhaidi kuendelea kushirikiana naa Jeshi hilo katika masuala ya usalama na ulinzi wa watoto kituoni hapo.

Posted in

Leave a comment