Na Issa Mwandagala, Songwe

Askari wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Songwe wametakiwa kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii kwa kuzingatia maadili ya kazi wakati wakitekeleza majukumu yao ya kusimamia sheria za usalama barabarani ili kuendelea kujenga taswira nzuri kwa Jeshi la Polisi.

Hayo yameelezwa Leo na Afisa Mnadhimu wa Polisi Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Akama Shaaban wakati akiwapongeza askari wa kikosi hicho kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuhakikisha hali ya usalama barabarani inaendelea kuimarika kwa watumiaji wa barabara Mkoni humo.

“Najua mnatambua moja kati ya maadili ya Jeshi la Polisi ni kufanya kazi kwa kuzingatia utoaji wa huduma bora kwa mteja ambapo ni pamoja na kutumia lugha nzuri wakati mnapowahudumia wateja hao ili kujenga taswira chanya na Wananchi waendelee kuliamini jeshi letu” alisema ACP Akama.

Mkuu wa Operesheni Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Nicholaus Livingstone alisema rushwa sio maadili ya Jeshi la Polisi na ni kitendo ambacho kinatia doa na kulichafua Jeshi.

“Rushwa inaondoa Imani ya wananchi kwa jeshi la polisi, ninawataka kutojihusha nayo ili kuendelea kuilinda taswira chanya ya Jeshi letu”, alisema ACP Livinstone.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Songwe, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Joseph Bukombe aliwapongeza askari hao kwa kuendelea kutoa elimu kwa madereva wa vyombo vya moto pamoja na watumiaji wa barabara juu ya matumizi sahihi ya barabara ikiwa ni pamoja na kutii sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika mkoani humo.

Posted in

Leave a comment