Na Mwandishi Wetu

Wito umetolewa kwa taifa na jumuiya za kimataifa kuchukua hatua za haraka kudhibiti ongezeko la taka za plastiki ambazo ni miongoni mwa changamoto kubwa za kimazingira zinazoikumba dunia kwa sasa.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya siku ya Mazingira Duniani yaliyoambatana na usafi wa mazingira na yaliyoandaliwa na Shirika la Haki za Binadamu na Utunzaji  Mazingira (HUDEFO), mwakilishi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) nchini Tanzania, Clara Makenya, alisema tani milioni 450 za taka za plastiki huzalishwa duniani kila mwaka.

Alisema   iwapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa mapema ifikapo mwaka 2050 bahari zitakuwa na plastiki nyingi kuliko samaki.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais nchini, Tanzania inazalisha kati ya tani milioni 14.4 hadi 20.7 za taka ngumu kila mwaka sawa na wastani wa kilo 241 hadi 347 kwa kila mtu kwa mwaka.

Miongoni mwa taka hizo, asilimia 12 ni taka za plastiki ambazo ni takribani  kati ya tani milioni 1.73 hadi 2.48 kwa mwaka wakati ni asilimia 5 hadi 10 pekee ya taka zote zinazozalishwa nchini ndizo zinazorejelewa kwa sasa licha ya kwamba asilimia 70 ya taka hizo zinaweza kurejelewa.

“Taka za plastiki ni janga la dunia, zinaharibu mazingira, zinatishia uhai wa viumbe vya majini na hata afya ya binadamu kwa kuchangia magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Makenya.

Alisema kuna haja ya kushirikiana kwa nguvu zote serikali, mashirika, sekta binafsi na jamii kupunguza uzalishaji wa plastiki kwa kuzirejeleza na kuhakikisha sheria za mazingira zinasimamiwa ipasavyo sanajli na utoaji wa elimu kwa umma ili kuachana na tabia ya kutupa taka ovyo.

Katika kutekeleza wajibu huo, Shirika la Catholic Relief Services (CRS) limesema linatekeleza mradi wa kuchochea uchumi mzunguko katika wilaya tatu za Mkoa wa Kigoma.

Meneja wa Programu wa CRS, Roberts Muganzi, alisema mradi huo unalenga kuelimisha jamii kuhusu usimamizi wa taka, kuanzisha mifumo ya urejelezaji, na kushirikiana na taasisi za kifedha kusaidia wabunifu wa bidhaa za plastiki.

“Licha ya kutoa elimu kwa jamii, tumetenga shilingi bilioni nne kwa ajili ya kuwasaidia wabunifu wenye mawazo ya kuzalisha bidhaa bora kutoka taka za plastiki ili kuongeza thamani ya plastiki badala ya kuziacha zichafue mazingira,” alisema Muganzi.

Asasi isiyokuwa ya kiserikali inayojihusisha na Haki za Binadamu na Utunzaji wa Mazingira (HUDEFO) imeendesha zoezi la usafi katika eneo la Bwalo la Maafisa wa Polisi , Masaki, ambapo washiriki 264 walijitokeza kukusanya taka za plastiki katika maeneo yanayozunguka bahari.

Mkurugenzi wa HUDEFO, Sara Pima alisema asasi yake inaendelea kuhamasisha uchumi rejelezi na kutoa mafunzo kwa vijana kuhusu namna ya kutumia taka kama fursa ya kiuchumi.

Alisisitiza umuhimu wa serikali kuwatambua rasmi wakusanyaji wa taka na kuwawekea mifumo rafiki ili waweze kufanya kazi yao kwa ufanisi zaidi.

“Wakusanyaji wa taka ndio jeshi la kwanza katika mapambano dhidi ya uchafuzi wa mazingira, lakini bado hawajatambuliwa ipasavyo na wito wetu kwa serikali kuwawekea mazingira bora ya kazi,” alisema Pima.

Kwa uapande wake, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Uzingatiaji na Utekelezaji wa Sheria kutoka Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Jamali Baruti, alisema serikali inaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria na kuhamasisha uwekezaji katika viwanda vya urejelezaji wa taka ili kudhibiti changamoto hiyo na kutoa fursa ya ajira.

Wadau wanasema si wakati wa kusubiri, dunia iko katika hatari ya kupoteza rasilimali muhimu kama maji safi, samaki, na afya ya jamii iwapo suala la taka za plastiki halitapewa uzito unaostahili.

Asasi ya HUDEFO kwa kushirikiana na NABU International imezindua ripoti mpya ya tathmini ya mfumo wa kisheria kuhusu Uwajibikaji wa Wazalishaji (EPR) ikieleza kuwa zaidi ya tani 29,000 za plastiki zimeripotiwa kuwepo baharini, mito na maziwa nchini mwaka 2018 pekee  zikiathiri maisha ya viumbe wa majini na usalama wa chakula.

Ripoti inaonesha kuwa licha ya Tanzania kuwa na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA), hakuna mwongozo madhubuti wa kulazimisha wazalishaji wa plastiki kuwajibika kwa taka zinazotokana na bidhaa zao.

Hali hiyo imesababisha mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro na maeneo ya mengine ya Pwani kujaa taka, huku wachukuzi taka wakifanya kazi ngumu bila kutambuliwa kisheria.

Takwimu zinaonyesha kuwa ni viwanda vichache tu vinavyotekeleza wajibu wao kama watengenezaji (EPR) kwa hiari, hali inayokwamisha juhudi za kupunguza taka za plastiki.

Ripoti inapendekeza Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004 kusimamiwa ipasavyo kwa kuweka mfumo wa lazima wa urejeshaji wa bidhaa (take-back system), na kuwatambua rasmi wachukuzi taka.

Inahimiza haki ya mazingira safi ijumuishwe katika Katiba ya Tanzania huku pia ikiitaka serikali kuendelea kushirikiana na sekta binafsi kutunga kanuni madhubuti.

Posted in

Leave a comment