
Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka watafiti na wataalamu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kufanya upembuzi yakinifu ili kubaini mahitaji halisi ya huduma za afya nchini.
Waziri Mkuu Majaliwa alitoa kauli hiyo juzi wakati wa kongamano la 13 la kisayansi la chuo hicho lililofanyika kwa siku mbili juzi na katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila jijini Dar es Salaam.
Alisema mapendekezo hayo yawasilishwe serikalini na kuzitaka Wizara za Afya, Elimu na Ofisi ya Rais, TAMISEMI kushirikiana na MUHAS kupanga namna bora ya kuboresha mitaala ambayo itakayosaidia kuzalisha wataalam mahiri kwenye tafiti za dawa, chanjo na vifaa tiba.
Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa serikali kupambana na magonjwa yasiyoambukiza na uboreshaji wa huduma za afya, ambapo kupitia MUHAS wataalam na watafiti wengi wamezalishwa na wanalisaidia taifa.
Alisema kuna umuhimu wa sekta za umma na binafsi kujadiliana kwa kina na kupitia machapisho ili kuishauri serikali namna ya kuongeza ushiriki wa wananchi katika vita dhidi ya magonjwa na imani imani potofu.
Alisema wakati tunajivunia upatikanaji wa huduma bora za afya nchini, mageuzi ya viwanda yanayochangiwa na ukuaji wa teknolojia yameleta chachu ya kuimarisha mifumo na ubora wa sekta za afya kote duniani suala linalotia moyo.
“Tunafarijika kuona taasisi zetu za vyuo vikuu na zinazotoa huduma zinajitahidi kwenda kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia ikiwa ni pamoja na utumiaji wa akili bandia,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia, anayeshughulikia Teknolojia na Elimu ya Juu, Prof. Daniel Mushi, alisema Chuo hicho kimeendelea kuwa kinara wa mabadiliko katika elimu ya afya, si tu kwa kutoa mafunzo bora, bali pia kwa kuchangia katika kufanya maamuzi ya kisekta yanayozingatia ushahidi.
Alisema wanatambua na kuthamini mchango wa Chuo hicho katika kuanzisha na kuendeleza majukwaa hayo ya kisayansi ambayo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha mawasiliano kati ya wanasayansi na watunga sera hivyo kuendeleza maendeleo yenye msingi wa kisayansi.
Alieleza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inahakikisha maeneo ya kujifunzia kwa vitendo yanapatikana ili kuongeza tija ya miradi mikubwa ya kimkakati pamoja na shughuli mbali mbali zinazofanywa na chuo hicho.
“Uwekezaji wa teknolojia katika matumizi ya Tehama umesaidia kuleta mageuzi kwenye sekta ya afya na kurahisisha utoaji wa huduma na MUHAS imekuwa kinara kwenye matumizi hayo na upatikanaji wa matokeo chanya,” alisema Prof. Mushi.
Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, alisema kongamano hilo liliwaleta pamoja watafiti na wadau ili kujadili na kutoa mapendekezo kwa kutumia bango kitita ili Wizara ya Afya ione fursa za namna inavyoweza kutumia teknolojia katika utoaji wa huduma na mafunzo katika sekta ya afya ili kuimarisha afya za wananchi.
Kwa upande wake, Naibu Makamu wa Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Utafiti na Ushauri wa Kitaalamu Prof. Bruno Sogoye, alisema kongamano hilo lilihudhuriwa na watafiti na wataalamu zaidi ya 200 kutoka ndani na nje ya nchi.
watafiti hao waliwasilisha tafiti zao kwenye maeneo nane ambavyo ni magonjwa yasiyoambukiza, afya ya mama na mtoto, ubunifu katika kuboresha maisha ya wananchi, magonjwa yanayoambukiza kama vile malaria na Ukimwi, mifumo ya afya pamoja na lishe.
Kwa mujibu wa Profesa Sogoye kongamano hilo lilihusisha watafiti kutoka nchi za Marekani, Norway, Kenya na wenyeji Tanzania.
Leave a comment