Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas More Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es salaam, Padre Aidan Mubezi na watoto waliopata sakramenti ya Kipaimara Siku ya Jumamosi jijini Dar es salaam mara baada ya adhimisho la misa takatifu ya kipaimara Parikiani hapo, (Picha na Francis Mpepo).

Na Vincent Mpepo

Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo amesema umaskini na utajiri kiroho unahusisha namna ambavyo mkristo ana uhusiano na Mungu na kwamba umaskini wa mali siyo siyo tatizo hapa duniani.

Mwadhama Kadinali Pengo alieleza hayo juzi wakati wa adhimisho la misa takatifu ya kipaimara katika Parokia ya Mt. Thomas More -Mbezi Beach Jimbo Kuu la Dar es salaam ambapo vijana 22 walipokea sakramenti ya Kipaimara,

Alisema kipaimara ni kumbukumbu halisi ya siku ya Pentekoste ambapo mitume walijazwa Roho Mtakatifu na kuata nguvu ya kueneza injili na kwamba baada ya kupakwa mafuta kwa wanakipaimara hao 22 wanapaswa kufanya kazi ileile ya kupeleka injili duniani.

“Kwa sakramenti ya Kipaimara mnajazwa Roho Mtakatifu na kupewa majukumu ya kuhubiri habari njema kwa maskini kama alivyofanya Kristo mwenyewe” alisema Mwadhama Pengo.

Alisema leo hii ukienda kuwahubiri maskini habari njema watadhani ni mradi au utawapa fedha kitu ambacho si sahihi.

Akirejelea maneno ya Mtakatifu Agustino, Mwadhmama Pengo alisema wakristo wengi wa sasa hudhani kuwa wao si maskini kwa kuwa wana pesa, chakula na mahali pa kuishi na kusisitiza kuwa umaskini unaotajwa kiiroho ni hali ya mwanadamu kutokuwa na mahusiano na Mungu.

“Huenda sisi ni maskini zaidi ya wanaolala nje kwa kukosa mahali pa kulala, chakula na mahitaji mengine”, alisema Kadinali Pengo.

Alisema matajiri wanaweza kutoa sadaka au vitu ghali likini wanasahau neno la Mungu na kwamba utajiri wa kweli ni ule wenye uhusiano na Mungu.

“Umaskini halisi ni ule wa kutokuwa na uhusiano mzuri na Mungu”, alisema Kadinali Pengo.

Aidha, Kadinali Pengo alielezea masikitiko yake kutokana na wanadoa kuachana baada ya miaka mingi ya kuishi pamoja na kusema kuwa si jambo jema na kwamba ni kinyume na mpango wa Mungu.

Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Thomas More Mbezi Beach, Jimbo kuu la Dar es salaam, Padre Aidan Mubezi alisema nia za ibada siku hiyo kuwa ni adhimisho la misa takatifu ya kipaimara na pongezi kwa Kadinali Pengo kwa kutimiza miaka 54 ya upadre.

Alisema Kadinali Pengo alifika Parokiani hapo Mwaka 2015 kwa Kipaimara cha kwanza na juzi alifika kwa Kipaimara cha kumi.

Alitumia fursa hiyo kumpngeza kwa kutimiza miaka 54 ya upadre na kuongoza waumini katika utoaji wa salamu za pongezi kwake.

Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo akimpaka mafuta mmoja wa watoto Daniela Francis wakati wa adhimisho la misa takatifu ya kipaimara Parokiani hapo, nyuma yake ni msimamizi wake (Picha na Francis Mpepo).

Mmoja wa watoto akipokea sakramenti ya ekaristi takatifu kutoka kwa Askofu Mkuu Mstaafu wa Kanisa Katoliki, Mwadhama Polycarp Pengo wakati wa adhimisho la misa takatifu ya kipaimara Parokiani hapo, nyuma yake ni msimamizi wake (Picha na Francis Mpepo).

Posted in

Leave a comment