
Na Mwandishi Wetu
Mtangazaji mstaafu wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Edda Sanga, ameelezea kukerwa na utangazaji wa mzaha na ucheshi unaovunja miiko ya tasnia hiyo kwa kuwa madai kuwa studio ni eneo la kuheshimiwa sio kupiga kelele au kurushiana maneno.
Sanga alitoa kauli hiyo jana wakati wa mafunzo kwa watangazaji chipukizi kutoka vyuo vya kati, yaliyoandaliwa kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 74 ya utangazaji Tanzania.
Alisema heshima ya utangazaji imepungua kwa sababu baadhi ya walipewa nafasi za utangazaji hawana wala maadili jambo linalosababisha wasikilizaji kuacha kufuatilia vipindi na maudhui kwa ujumla.
“Studio ni eneo la heshima, utangazaji sio kupiga kelele wala eneo lakurushiana maneno,” alisema Sanga.
Akizungumzia eneo la uandaaji wa maudhui katika vipindi vya mahojiano, Sanga alisema lina udhaifu mkubwa kwa sababu baadhi ya waandishi wa habari hususani wa kizazi kipya,hawajiandai wanapotaka kufanya mahojiano na kuzalisha maudhui ambayo hailengi kuisaidia jamii.
Alisema suala la waandishi wa habari kushindwa kuwatafuta watu mahususi ambao ni vyanzo vya kuaminika kuzungumzia mada badala yake huwatumia wale wanaopatikana mara kwa mara na kushauri kuwatafuta watu wenye weledi na maarifa ya kuzunngumza mada husika.
“Eneo la mahojiano bado lina changamoto kwa baadhi ya waandishi hawajiandai ipasavyo, wala hawatafuti watu sahihi wenye ujuzi wa kuzungumzia mada husika hivyo kuathiri ubora wa taarifa zinazozalishwa,” alisema Bi Edda.
Katika mafunzo hayo, washiriki walijadili kuhusu hali ya kizazi kipya katika kulinda maadili ya kitaifa na uzalendo ambapo wazungumzaji walieleza hofu yao juu ya kupotea kwa misingi ya mshikamano wa kijamii kutokana na mabadiliko ya kiteknolojia.
Balozi Christopher Liundi, alisema kukosekana kwa uzalendo miongoni mwa vijana kunachangiwa na kutopatiwa elimu mapema kuhusu umuhimu wa suala hilo,pamoja na athari zamatumizi ya simu na mitandao ya kijamii.

“Siku hizi rafiki mkubwa wa watu amekuwa ni simu hakuna tena upendo wa kweli wala urafiki wa dhati kama zamani, watu hawatembeleani, hawatafutani tena kama enzi zetu,” alisema Balozi Liundi.
Alisema redio na vyombo vya habari kwa ujumla vina nafasi kubwa ya kusaidia kurejesha maadili ya kijamii, lakini hilo linawezekana tu endapo watangazaji na waandishi wa habari watafanya kazi zao kwa kuzingatia weledi, maadili na dhamira ya kuelimisha jamii.
Debora Mwenda ni miongoni mwa waandishi wakongwe tangu uhuru alisema anakerwa na baadhi ya matamshi ya baadhi ya watangazaji wa kisasa ambao hushindwa kutamka majina ya nchi ikiwemo Tanzania na miji mingine mikubwa duniani.

Mjumbe wa Bodi ya Chama cha Watangazaji Wakongwe wa Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), Judica Losai alisema kutokana na kukua kwa teknolojia kunahitajika kuandaliwa vipindi au maudhui inayotumia dakika chache ikiwa na ubora unaotakiwa ili kumvutia msikilizaji.

Leave a comment