Na Vincent Mpepo

Watangazaji wakongwe wa iliyokuwa Redio Tanzania Dar es salaam (RTD) ambayo kwa sasa ni sehemu ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) wametumia siku ya maadhimisho ya miaka 74 ya utangazaji Tanzania kubalishana uzoefu na waandishi wa habari watangazaji chipukizi ili kuhakikisha wanarithisha amali njema katika tasnia ya hiyo.

Wakizungumza wakati wa mafunzo ya siku moja yaliyofanyika jana katika Ukumbi wa Break Point Kijiji cha Makumbusho jijini Dar es salaam, wakongwe hao wamesema licha ya kukua kwa sayansi na teknolojia kunakoigusa tasnia ya habari hususani utangazaji misingi ya uandishi wa habari haijabadilika.

Akifungua mafunzo hayo, Mwenyekiti wa Chama cha Wakongwe wa Redio Tanzania Dar es salaam, Suleiman Kumchaya alisema madhumuni ya mafunzo hayo ni kubadishana mawazo na waandishi wa habari watangazaji kwa kuelezea uzoefu waliokuwa nao kwa miaka kadhaa kama sehemu ya mchango wao kwa tasnia ya habari.

“Unapojali kazi yako siku zote utasikiliza na kufuatilia kinachoendelea katika tasnia yako”, alisema Kumchaya.

Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya chama hicho, Balozi Mstaafu, Christopher Liundi alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa waandishi wa habari watangazaji kwa kuwa yatasaidia kurudisha taaluma hiyo katika misingi lakini imekuwa fursa nzuri ya pamoja kujadili changamoto na fursa zilizopo.

Balozi Liundi alisema msingi wa taaluma ya uandishi wa habari umejikita katika kulinda maslahi ya umma kwa kuwa wafanyacho kila seku ni sehemu ya elimu waitowayo na hawana budi kujiongezea maarifa kila iitwapo leo na ndio maana hata miundo ya ajira na kiserikali inatambua suala hilo.

“Uandishi wa habari ni taaluma yenye mifumo yenye viwango vya juu vinavyofahamika na kupimika hivyo ni muhimu kwa waandishi kuiheshimu kwa kufuata taratibu, kanuni na sharia ambazo kila mhusika atawajibika kwazo”, alisema Balozi Liundi.

Alisema ni muhimu kwa waandishi watangazaji kuzingatia misingi ya taaluma hiyo inayowataka wawajibike kwa umma kwa uadilifu unaozingatia usahihi, umahiri na weledi katika kazi zao.

Makamu Mwenyekiti wa Wakongwe RTD, Jacob Tesha alizungumzia changamoto ya maudhui ya vyombo vya habari kutoka nje yanayotumiwa na baadhi ya vyombo vya habari na athari zake katika utamaduni wetu na kuwataka waandishi wa habari wasomi kuzalisha vipindi vyenye asili ya kitanzania ili kulinda utamaduni wetu.

Kwa upande wake Mkufunzi wa Masomo ya Habari na Mawasilinao ya Umma kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Bujo Ambosisye aliwashukuru wakongwe hao kwa kujali na kujitoa kwao kwa ajili ya waandishi wa habari chipukizi na kwamba ni mara ya pili kwake kukutana na wakongwe hao katika mafunzo hayo.

‘Niliwahi kukutana na baadhi ya wakongwe katika tasnia ya habari miaka kadhaa ilyopita wakati wa maazimisho ya wiki ya ukombozi wa bara Afrika na kimsingi tunanafaika sana na uwepo wenu”, alisema Ambosisye.

Katika mafunzo hayo mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo misingi ya uandishi wa habari za redio, uandishi wa habari za redio kabla na baada ya maendeleo ya teknolojia, changamoto katika kipindi kisichokuwa cha uchaguzi na kipindi cha uchaguzi.

Posted in

Leave a comment