
Na Vincent Mpepo
Makamu Mkuu wa chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Alex Makulilo amewataka wafanyakazi wa chuo hicho kubadilika kifikra na kiutendaji ili kuendana na ushindani katika mifumo ya uendeshaji taasisi za elimu ya juu kutoka ndani na nje ya nchi.
Profesa Makulilo alitoa wito huo jana wakati wa mkutano wake wa kwanza na wafanyakazi wa chuo hicho akihudumu kwa nafasi hiyo mara baada ya uteuzi wake mapema Mwezi Juni, 2025.
Alisema sura ya elimu ya juu hivi sasa imebadilika sana na kwamba kwa kuangalia mwenendo wanaweza kuelewa kinachoendelea huku mabadiliko hayo yakiathiri soko la chuo hicho.
“Idadi ya vyuo vikuu na vyuo vikuu huria imeongezeka kwenye nchi ambazo hazikuwa navyo”, alisema Profesa Makulilo.
Alisema idadi ya wanafunzi wa kimataifa kutoka nje ya nchi imepungua akitolea mfano wa idadi ya wanafunzi wa uzamili kutoka Kenya kwa mwaka wa masomo wa 2022/2023.
“Takwimu zinaonesha idadi ya wanafunzi wa uzamili kutoka Kenya imepungua kutoka wanane (08) hadi sita (06) maana yake ushindani umeongezeka”, alisema Profesa Makulilo.
Aidha alizungumzia ushindani kutoka ndani ambao umetokana na vyuo vikuu vingine hapa nchini kutoka kwenye mfumo wa mazoea wa madarasa na kuingia kwenye mfumo wa elimu huria na masafa yaani (ODL).
“Wengine wameenda mbele zaidi na kuanza kujenga vituo vya mikoa na wanaviita majina kama kampasi za kilimo, elimu bahari au madini na kadhalika”, alisema Profesa Makulilo.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Josiah Katani aliwakumbusha wafanyakazi wa chuo hicho taratibu za utumishi wa umma ikiwemo kuwahi kazini, kuomba ruhusa wanapokuwa safari au kukumbwa na changamoto yoyote.
“Barua zinazoenda uongozi wa juu lazima zipitishwe kwa msimamizi wako wa kazi”, alisema Profesa Katani.
Aliwaasa watumishi kuomba likizo kwa kutumia mfumo, kuhakiki taarifa zao na waende likizo kwa tarehe walizojaza kwenye kwenye mfumo na ikitokea kuna mabadiliko ni lazima wapate kibali kwa uongozi.
Profesa Katani aliwakumbusha wafanyakazi wa chuo hicho kujaza kujaza kwa wakati majukumu yao katika mfumo wa usimamizi wa utendaji kazi katika utumishi wa umma yaani (PEPMIS)ili kuondokana na adha ya kutopanda vyeo.
“Alama za chini kabisa kwa mfanyakazi ni 75%”, alisema Profesa Katani.
Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Utafiti wa Ushauri wa Kitaalamu, Profesa Saganga Kapaya aliezea maendeleo ya uhuishaji na utengenezaji wa mitaala na kubainisha kuwa zoezi hilo linaendelea vizuri.
Alisema idadi ya mitaala ya programu katika shahada za awali, uzamili na uzamivu zilizowasilishwa Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania ni 109 baada ya kupitishwa kwenye kamati za maamuzi za juu za chuo hicho.
Aidha aliwataka wafanyakazi wa chuo hicho kuboresha huduma kwa mteja ili kutoa huduma nzuri zitakazowafanya wanafaunzi waliodahiliwa kuendelea na masomo chuoni hapo badala ya kuhama au kuacha.
Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za. Elimu ya Juu Tanzania tawi la Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Salatiel Chaula akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wa chuo hicho alisema wamepokea maelekezo wapo tayari kwa utekelezaji ili kusukuma mbele gurudumu la taasisi hiyo.

Leave a comment