Na Vincent Mpepo

Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Mtaa wa Kwembe wameelezea mafanikio, fursa na changamoto zinazowakabili katika safari ya kujikwamua kichumi kama sehemu ya jamii huku wakitoa rai kwa washarika na jamii kuwaunga mkono katika harakati zao.

Hayo yamebainishwa na Mwenyekiti wa Vijana Mtaani hapo, Abel Mvungi Siku ya Jumapili ambayo kwa kalenda ya KKKT ilikuwa ni Siku ya vijana ambapo vijana hao walitumia siku hiyo kuonesha talanta zao katika maonesho ya kazi za mikono, bidhaa na huduma wazitoazo kama sehemu ya shuhguli wazifanyazo ili kukuza mfuko wao na kujikwamua kichumi.

Alisema pamoja na kumtumikia Mungu katika utume na shughuli mbalimbali za kikanisa wanahitaji kuungwa mkono na washarika na jamii ya wanakwembe ili waendelee kuwa imara kiuchumi na hivyo kupunguza utegemezi kwa wazazi na walezi.

“Tunaomba muendelee kutushika mkono katika miradi mbalimbali ikiwemo huu wa matunda na mbogamboga ili kuisukuma mbele idara ya vijana katika kutekeleza malengo yake ya kuwainua vijana”, alisema Abel.

Akizungumzia mafanikio ya umoja huo mtaani hapo, alisema wa Mwaka jana 2024 umoja huo ulifanikiwa kuhudhuria Kongamano la vijana jijini Arusha amabalo lililenga kuwafundisha vijana kumjua Mungu na namna bora ya kuishi katika jamii inayowazunguka.

“Viongozi walipata safari ya kwenda Dodoma kwa ajili ya kongomano la kiuongozi”, alisema Abel.

Alibainisha mafanikio mengine kuwa ni kuwawezesha vijana 103 kushiriki Tamasha la Twen’zetu kwa Yesu lililofanyika Kawe jijini Dar es salaam na kuwashukuru washarika wa Mtaa huo kwa kuwaunga mkono katika ununuzi wa tiketi kwa baadhi ya vijana ili washiriki katika kongamano hilo.

Alisema Mwaka 2024 umoja huo uliazimia kuanzisha mradi wa pikipiki tatu yaani bodaboda kwa kufanya harambee ndogo Tarehe 7/7/2024 ambazo zingetumiwa na vijana kanisani kama sehemu ya ajira na kuuzalishia mfuko wa vijana fedha. 

“Katika harambee hiyo tulifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi 1,300,000/ taslimu na ahadi za shilingi 2,600,000/ ambazo hazijalipwa mpaka leo hivyo kufanya mradi huo kutokufanikiwa kwa wakati”, alisema Abel.

Mhubiri wa siku hiyo, Kresensia Kabala alizungumzia umuhimu wa vijana kuwa na nidhamu katika kila walifanyalo kwani kupitia nidhamu ndio inaonesha thamani ya ujana katika jamii  kinyume na hilo ni kuonekana hawafai.

“Jitengenezee mazingira yatakayowakosesha watu na jamii sababu za kukukudharau”, alisema Kresensia.

Aliwataka vijana kufanya kazi na wakati mwingine kutochagua kazi hata kama wamesoma hususani wakati huu ambapo kuna changamoto ya upatikanaji wa ajira.

Aidha aliwaasa wazazi kuwafundisha kazi watoto wao ili waweze kujitegemea badala ya kuwalea kama mayai kitu ambacho ni janga katika masiha yao ya baadaye kama akina baba na akina mama watarajiwa.

“Matatizo mengi katika ndoa yanatokana  na msingi mbovu wa malezi katika familia”, alisema Kresensia.

Aliwaasa vijana wa kike na wa kiume wanaosoma kutumia vizuri muda wao shuleni na vyuoni katika kuandaa kesho yao na kuacha tamaa kwani itasababisha upotevu wao na kuwapa majonzi wazazi na walezi amabao hutumia rasilimali zao kuhakikisha wanapata elimu.

Mchunganji Dkt. Mwatumai Mwanjota alihudumu katika ibada hiyo na huduma za kichungaji kadhaa zilifanyika ikiwemo ubatizo na huduma ya chakula cha Bwana.

Siku hiyo ilipambwa na uimbaji kutoka kwa vijana huku huduma zote kanisani hapo zikiendeshwa nao jambo  lililoonesha hazina kubwa ya talanta na vipawa mbalimbali kwa vijana hao ambao wakipewa nafasi wanaweza kuidhihirishia jamii thamani yao.

Posted in

Leave a comment