Na Rehema Kavishe

Waandishi wa habari chipukizi wametakiwa kusoma kwa bidi ili kuwa na maarifa stahiki katika fani hiyo yatakayowawezesha kuendana na ushindani wa soko la ajira na ikibidi kuwa wajasiriamali katika maeneo mbalimbali ya tasnia hiyo.

Hayo yamejiri wakati wa ziara ya Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Vincent Mpepo katika Chuo cha ‘Spring Institute of Business and Science’ hivi karibuni Mkoani Kilimanjaro ambapo aliwaasa mambo kadhaa ikiwemo faida za kujiendeleza kitaaluma.

Akizungumza na wanafunzi wanaosomea fani ya uandishi wa habari na utangazaji chuoni hapo aliwataka kusoma kwa bidi ili kuhumili ushindani na kujiongezea wigo wa upatikanaji wa ajira na kujitengenezea fursa kwa ajili ya masomo ya juu.

“Jitahidi uwe na ufaulu mzuri kuanzia GPA ya 3 ambayo ndiyo sifa ya kudahiliwa kusoma shahada awali”, alisema Mpepo.

Pamoja na ushauri huo, Mpepo aliwasilisha vitabu vya masomo ya habari na utangazaji vitakavyowasaidia kujiongezea maarifa na maandalizi ya mitihani yao.

Mwanafunzi wa stashahada ya uandishi wa habari na utangazaji chuoni hapo, Careen Kisanga alisema wamepokea vitabu hivyo na wanatoa shukrani kwa mhadhiri huyo.

Mkuu wa Idara ya Uandishi wa Habari na Utangazaji chuoni hapo, Amos Majaliwa aliwakumbusha wanahabari wanafunzi hao kuwa na nidhamu katika masuala ya kitaaluma ili kuwa na matokeo mazuri kinadharia na vitendo ambayo ndiyo mtaji mzuri katika soko la ajira.

“Ni muhimu mfanye vizuri ili kuwa na viwango vizuri vya ufaulu kwa asilimia 80 au 90”, alisema Majaliwa.

Alisema uvivu na kutokujifunza kwa bidii ni vikwazo dhidi ya malengo mazuri wanayojiwekea na kusisitiza kuwa mafanikio katika taaluma hutegemea juhudi binafsi na kujituma.

Kwa upande wake mwanafunzi wa mwaka wa pili katika fani ya uandishi wa habari na utangazaji chuoni hapo, Juliani Kimaro alielezea umuhimu wa kujiendeleza kitaaluma katika tasnia hiyo na kuwa ataongeza bidii ili kufikia maleongo yake.

Aidha alielezea kufurahishwa na ziara ya mhadhiri huyo kwani wamepata uzoefu wa fursa mbalimbali zilizopo katika tasnia ya habari, sifa na vigezo vya kujiunga na masomo ya shahada katika Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

“Leo tumepata uelewa kwa kuwa tumejifunza kuwa uandishi wa habari si kazi tu bali, ni taaluma yenye uzito na majukumu makubwa kwa umma,”, alisema Juliani.

Posted in

Leave a comment