

Na Issa Mwadangala
Wazazi na walezi wa Kijiji cha Ikonya kilichopo Kata ya Bara Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe wametakiwa kuhakikisha malezi ya watoto yanazingatia maadili ya dini.
Hayo yamesemwa na Naibu Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa wa Songwe Mrakibu wa Polisi (SP) Ester Ngaja juzi wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa paa la Kanisa Katoliki Kigango cha Ikonya ambapo aliwataka waumini wa Kanisa hilo kuwalea watoto kwa kuzingatia mafundisho ya dini ili kuwaepusha kujiingiza katika tabia za kihalifu.
“Kanisa linapaswa kuwa mahali sahihi kwa malezi kwa kushirikiana na familia na jamii kwa ujumla,” alisema SP Ngaja.
Katika hafla hiyo ya harambee, ikiongozwa na mmoja wa wazaliwa katika kata hiyo Bi Mariam Nzowa alisema kuwa baada ya kutembelea kanisa hilo alikuta changamoto ya waumini kukosa sehemu ya kusalia kutokana na kanisa kutokuezekwa ndipo alipochukua hatua ya kufanya harambee ili kukusanya kiasi cha shilingi milioni saba (7) kwa ajili ya kutatua changamoto hiyo.

Tukio hilo lilihudhuriwa na viongozi wa dini, wanajamii na wageni mbalimbali walioungana kwa moyo mmoja katika kuchangia maendeleo ya kanisa.
kwa upande wake Padre wa Parokia ya Bara Attilio Mbogela aliwapongeza waumini wa Kijiji cha Ikonya kwa mshikamano wao na moyo wa kujitolea katika kazi za maendeleo na kuhimiza waendelee kudumisha upendo, mshikamano na heshima kwa taasisi za kidini.

Aidha, alilishukuru Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe na mgeni rasmi Bi. Mariam Nzowa kwa ushirikino na mchango mkubwa katika mafanikio ya harambee hiyo huku akiahidi kuendelea kushirikiana na jamii na viongozi wa serikali katika kuimarisha maadili mema miongoni mwa waumini na jamii kwa ujumla.
Leave a comment