Na Vincent Mpepo

Wadahiliwa wapya wa shahada za uzamili na uzamivu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kituo cha Mkoa wa Dodoma wametakiwa kutumia muda vizuri ili kuhakikisha wanamaliza programu walizodahiliwa ndani muda uliopangwa.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kituo cha Mkoa cha Dodoma, Dkt. Mohamed Msoroka wakati wa ufunguzi na uwasilishaji wa mafunzo elekezi yaliyofanyika Jumamosi katika ukumbi wa mitihani wa kituo hicho na kuhudhuriwa na wanafunzi wa shahada za juu waliodahiliwa katika fani mbalimbali.

 Alisema baada kudahiliwa na kukubali kusoma ni lazima wakubali kupunguza baadhi ya vitu au majukumu mengine ya kijamii ili watumie vizuri muda katika masomo.

“Wakati mwingine utalazimika kuacha posho za vikao, safari au shughuli za kijamii kama ndoa na nyinginezo ili utumie muda wako katika elimu”, alisema Dkt. Msoroka.

Aliwataka kufuata taratibu na maelekezo mengine kwa mujibu wa miongozo ya chuo ikiwemo kuwasiliana na wasimamizi wao wa utafiti katika safari yao ya elimu.

“Usikae na changamoto badala yake wasiliana na msimamizi wako upate ufumbuzi na ushauri wa namna ya kuendelea na masomo yako”, alisema Dkt. Msoroka.

Alisema furaha ya walimu, wakufunzi na wahadhiri ni kuona wanafunzi wao wanamaliza masomo yao kwani ni jambo la faraja badala ya kuona hawamalizi kwa wakati.

Akitoa mafunzo ya mifumo ya Tehama inayoyumika chuoni hapo kusomea na kujifunzia ya chuo hicho, Hassan Mwazema alisema mifumo hiyo inatoa nafasi nzuri ya mwanafunzi kupata huduma mbalimbali hata bila kufika ofisini kwa kuwa inasomana na mifumo mingine ya kitaifa ili kumhakikishia urahisi wa huduma.

“Uzuri ni kuwa mifumo yetu inasomana hivyo si lazima sana kuja ofisini kwetu kwa kuwa unaweza kufanya kila kitu mahali ulipo”, alisema Hassan.

Mdahiliwa wa Shahada ya Umahiri ya Sanaa katika Ushirikiano na Maendeleo ya Kimataifa (MAICD) choni hapo, Hafsa Lyimo alisema kama mama, mke na mzazi amependa kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kutokana na fursa ya kupangilia masuala mbalimbali ya kifamilia, kiofisi na kitaaluma na hivyo kuhakikisha kila kimoja kinapata muda wake.

“Kama mwanamke kitu kilichonileta kusoma Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni kuhakikisha kuwa na ndoto yangu inatimia”, alisema Hafsa.

Aliwataka wanawake kutumia fursa zilizopo katika eilimu badala ya ya kuwa na visingizio vingi ambavyo kimsingi havina uhalisia ili kutimiza ndoto zao ili kuongeza thamani ya maisha yao katika jamii.

Katika mafunzo hayo. wadahiliwa hao wa shahada za umahiri na uzamivu walifundishwa masuala mbalimbali ikiwemo namna ya kusoma katika mfumo wa elimu huria na masafa, namna ya kutumia mifumo ya Tehama ya chuo hicho na taratibu mbalimbali kuhusu wajibu wa wanafunzi na wasimamizi wa tafiti.

Posted in

One response to “Wadahiliwa Uzamili, Uzamivu Washauriwa Kutumia Vyema Muda”

  1. Regan Ifunya avatar
    Regan Ifunya

    Nawatakia kila lakheri wadahiliwa na viongozi wa chuo Kwa ujumla katika kutekeleza majukumu yao

    Like

Leave a comment