
Na Vincent Mpepo
Wakristo wametakiwa kufanya kila kitu wakitanguliza upendo kwani upendo huondoa changamoto mbalimbali katika maisha ya kimwili na kiroho.
Wito huo umetolewa na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, Obed Songoyo wakati akihubiri katika ibada Siku Jumapili, katika Mtaa wa Nambere, Usharika wa SokoniII Siku ya Bwana ya sita (06) baada ya Utatu ambapo alisisitiza kufanya kila kitu kwa upendo wa Yesu.
Mchungaji Songoyo alisema ikiwa wakristo na jamii kwa ujumla itafanya kila kitu kwa upendo kuna namna ambapo kila mmoja ataishi kwa kutimiza wajibu wake bila kumkwaza mwingine na kila mmoja ataishi kwa ajili ya mwingine.

“Neno la Mungu linasisitiza kuishi kwa kupendana kwa kuwa upendo ndio amri kuu”, alisema Mchungaji Songoyo
Alisema amri ya upendo ina upya ndani yake na upya huo ni kwa sababu imeongeza suala la kupenda watu wote wawe ni maadui au wasio maadui.
“Kipimo cha kupendana sisi kwa sisi ni Yesu mwenyewe”, alisema Mchungaji Songoyo
Alisema upendo wa kweli haushindwi na dhambi na kwamba watu huishi kwa kuvumiliana na kuchukuliana akitolea mfano wa mume na mke kuwa wanahitaji upendo wa kweli kwa kuwa mwisho wa siku wanahitajiana.
“Tukipendana sisi kwa sisi tunadhirisha kuwa sisi ni wakristo wa kweli”, alisema Mchungaji Songoyo.
Alisema kwa kawaida ya mila za kimasai upendo unatakiwa kuanzia nyumbani na kuwatahadharisha baadhi ya watu ambao huwapenda watu wa nje ya nyumba yao badala ya watu wa ndani na kusisitiza huo siyo upendo wa kweli.

Alisema wanandoa hawapaswi kuishi kihasara hasara bali wanapaswa kuishi kwa kuoneshana upendo ambao utawafanya kudumu katika ndoa kwa kuwa watavumiliana na kuchukuliana na kusisitiza kuwa kuishi bila upendo ni kinyume na maagizo ya Kristo.
Aidha aliwajulisha washarika mtaani hapo kuwa Mwinjilisti wa Mtaa huo ameteuliwa kwenda kuinjilsha Zanzibar na kuwataka wamuombee na kumuwezesha ili asiende kuwa mnyonge akiwa katika kazi ya Mungu.
Ibada hiyo iliongozwa kwa lugha ya kimasai na tafsiri ilitolewa kwa wageni ili waweze kufuatilia ujumbe wa neno la Mungu ambapo huduma kadhaa za kichungaji zilifanyika ikiwemo ubatizo wa wototo, kurudi kundin na chakula cha Bwana.

Leave a comment