Na Mack Francis

‎Zaidi ya vijana na viongozi wa mila wapatao elfu kumi kutoka jamii ya kifugaji ya Kimasai wamekusanyika katika viwanja vya Elerai, jijini Arusha, kutoa adhabu ya kimila kwa vijana wawili waliokiri kutumia lugha chafu dhidi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dk. Samia Suluhu Hassan, kupitia video iliyosambazwa mitandaoni.

‎‎Vijana hao, waliotambulika kwa majina ya Laurence Kuesoy na David Zakayo, wote wakazi wa Arusha, walijitokeza hadharani na kuomba radhi mbele ya umati mkubwa, wakielekeza msamaha wao kwa Rais Samia mbele ya wazee wa mila katika eneo la kimila la Elerai ambapo kila mmoja alitakiwa kulipa faini ya dume la ng’ombe kama njia ya kutubu na kurudisha heshima ya jamii.

‎‎Kwa mujibu wa viongozi wa kimila wa jamii ya Kimasai wakiongozwa na Laigwanani Mkuu, Isack Ole Kissongo, walieleza kuwa wamechukizwa sana na maudhui ya video iliyorekodiwa na vijana hao tarehe 20 Juni 2025, katika eneo hilo la kimila wakati wakifanya shughuli za usafi na kisha kuiweka kwenye mitandao ya kijamii ikiwa na maudhui yasiyofaa kwa kiongozi wa nchi.‎

‎Laigwanani Kissongo alisisitiza kuwa jamii ya Kimasai haikubaliani na tabia ya matusi kwa viongozi wa kitaifa, na kwamba hatua hiyo ya kutoa faini ni ya kimila, inayolenga kudumisha maadili, nidhamu na heshima kwa viongozi wa taifa.‎

‎Kulingana na hayo viongozi wa kimila waliomba radhi kwa niaba ya jamii ya Kimasai kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kumhakikishia Rais Samia kuwa jamii hiyo itaendelea kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha nidhamu, amani, na heshima kwa viongozi wa kitaifa.

‎‎Katika hatua nyingine, Laigwanani Mkuu Isack Ole Kissongo aliiomba serikali kuhakikisha kuwa eneo la kimila la Elerai lenye zaidi ya ekari 100, lililopo Kata ya Elerai, Mtaa wa Majengo, halivamiwi wala kugawanywa kiholela, kwa kuwa lina umuhimu mkubwa kwa shughuli za mila na utamaduni wa jamii hiyo.

Posted in

Leave a comment