
Na Mack Francis, Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Kenani Kihongosi na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Louise Young wamekubnaliana kuimarisha ushirikiano katika sekta ya afya na utalii mkoani Arusha.
Mazungumzo hayo yalifanyika hivi karibuni wakati Balozi Young akiwa ziarani mkoani humo, akiambatana na Mkuu wa Diplomasia ya Uchumi wa Ubalozi wa Uingereza nchini, Bi. Tammy Clayton.
Ujumbe huo wa Balozo wa Uingereza ulitemebelea na kukagua miradi mbalimbali inayofadhiliwa na Serikali ya Uingereza pamoja na kukutana na wawekezaji kutoka Uingereza waliopo Kanda ya Kaskazini, hususani katika sekta ya utalii.

Kihongosi alisema Mkoa wa Arusha unaendelea kuimarika katika miundombinu ya usafiri na utoaji wa huduma muhimu kwa wageni na watalii akisisitiza kuwa usalama na amani ni mambo yaliyotamalaki mkoani humo.
“Kwa sasa kupitia Programu ya TACTIC, tunaanza ujenzi wa zaidi ya kilomita 30 za barabara ndani ya jiji na katika maeneo ya hifadhi ya Ngorongoro ili kuboresha upatikanaji wa huduma na kurahisisha shughuli za utalii katika misimu yote ya mwaka”, alisema RC Kihingosi,
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa alisema ofisi yake iko wazi kwa kushirikiana na wadau wote wa maendeleo wakiwemo wawekezaji na wageni, kwa lengo la kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia watalii zaidi.
Balozi Young alipongeza jitihada za mkoa wa Arusha katika kukuza utalii na huduma za kijamii, huku akionesha utayari wa kuendelea kushirikiana na serikali ya mkoa katika maeneo mapya ya uwekezaji.
Alisema takribani watalii 80,000 kutoka Uingereza walitembelea Tanzania mwaka 2024, wengi wao wakifika Arusha na Zanzibar.

Balozi Young pia ametangaza mpango wake wa kurejea Arusha wiki ijayo pamoja na familia yake kwa ajili ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa ndani ya hifadhi ya Ngorongoro akieleza furaha yake juu ya mandhari na vivutio vya kipekee vya utalii vilivyopo mkoani humo.
Mhe. Kihongosi kwa upande wake alimhakikishia Balozi Young kuwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025 hautaathiri shughuli za utalii, huku akitoa wito kwa wageni wa ndani na nje ya nchi kuendelea kutembelea mkoa wa Arusha kutokana na uwepo wa vivutio vya utalii vyenye upekee.
Leave a comment