
Na Sylvester Onesmo-Dodoma
Mgombea urais wa Chama Cha Kijamii (CCK), David Mwaijojele, ameahidi iwapo atapewa ridhaa na watanzania kuiongoza nchi, serikali yake itahakikisha wafanyakazi wanajengewa nyumba wakiwa bado kazini ili kuondoa hofu ya maisha magumu baada ya kustaafu.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu ya kugombea urais akiwa na Mgombea mwenza Masoud Ali bdallah katika ofisi za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Mwaijojele alisema serikali ya CCK imejipanga kuweka mfumo wa makato maalum ya kodi kwa wafanyakazi walioko kazini ambayo yatatumika kuwajengea nyumba kabla hawajastaafu.
“Tumeona mara nyingi wafanyakazi waliopo kwenye ajira sasa hivi wanaogopa kustaafu kwa sababu ya mazingira wanayoishi mtu anafanya kazi miaka mingi lakini hana hata kiwanja, hana nyumba na anapofikiria kuacha kazi anajiuliza ataishije”, alisema Mwaijojele.
Alisema iwapo wananchi waiamini CCK na kuipa dhamana ya kuobgoza kitaweka mazingira wezeshi ya kuwakatia kodi kwa kiwango kidogo wakiwa kazini ili zisaidie katika ujenzi wa nyumba hizo kabla hawajastaafu.
Mwaijojele alionhgeza kuwa lengo la mpango huo ni kuandaa mazingira salama ya ustaafu kwa watumishi wa umma na sekta binafsi ili nafasi zao zichukuliwe na vijana huku waliostaafu wakiendelea kuishi maisha ya heshima na hadhi.
Sanjali na hilo, Mwaijojele alisema serikali ya CCK pia ina mikakati thabiti ya kuwawezesha wananchi wa kawaida kupitia mfumo wa kuweka akiba ya kiasi kidogo cha fedha, ambapo serikali itawaunga mkono kwa kuwapatia mitaji ya kujiendeleza.
“Hata kama mtu unaweka mia mia kwa siku, tunataka mwisho wa mwaka uweze kupata msaada kutoka serikalini hata kama una kibanda cha chumba kimoja, CCK itakusaidia uweze kukipanua hii ni kwa wafanyabiashara, wajasiriamali wadogo, wachimba madini, waandishi wa habari na wananchi wote kwa ujumla”,alisema Mwaijojele.
Akizungumzia mchakato wa kuchukua fomu, Mwaijojele aliishukuru Tume ya Taifa ya Uchaguzi kwa kuratibu zoezi hilo weledi akidai kuwa kuwa tume imekuwa ikishirikiana bega kwa bega na wagombea wote tangu hatua za awali.
“Ninawashukuru sana Mwenyekiti wa Tume, Mkurugenzi na jopo zima la Tume pamoja na wafanyakazi wote kwa kazi nzuri mnayoifanya tumekuwa tukishirikiana nanyi bega kwa bega katika kila hatua na tunathamini sana jambo hilo,” alisema Mwaijojele.
Mwaijojele alibainisha vipaumbele vya CCK kuwa ni kilimo cha kisasa, elimu, afya, ajira, pamoja na ustawi wa vijana na wazee.
Alisema CCK inalenga kuleta mageuzi ya kweli kwa watanzania wote kwa kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Leave a comment