Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tazania anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Josiah Katani ni miongoni mwa waliofika katika zoezi la upimaji afya mapema jana. Anayeonekana nyuma yake ni Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Francis Badundwa na Profesa Cosmas Mnyanyi. (Picha kwa hisani ya Dkt. Adamu Namamba).

Na Vincent Mpepo

Wafanayakazi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wametakiwa kujali afya zao kwa kupima na kupata ushauri wa kitabibu ili kujua changamoto zinazowakabili mahali pa kazi na namna ya kukabiliana nazo.

Mkurugenzi wa Rasilimali watu na Utawala wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Francis Badundwa alitoa wito huo jana ofisini kwake Kinondoni jijini Dar es salaam wakati wa mahojiano na mwandishi wetu na kuwataka wafanyakazi hao kutumia fursa ya siku tano ya uwepo wa watumishi wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kwa zoezi hilo la upimaji afya.

Alisema kumekuwa na mwitikio mdogo wa wafanyakazi katika zoezi hilo la upimaji licha ya kukiri kuwa masuala afya ni masuala binafsi.

“Natambua wengi huenda kipima hospitali moja kwa moja ambapo watapata vipimo, majibu na tiba”, alisema Badundwa.

Kwa upande wake, Dkt. Pricila Michael kutoka Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) alianisha majukumu ya taasisi yake kuwa ni ukaguzi wa afya unahusisha upimaji wa vipimo vya awali kwa mwajiriwa mpya, upimaji wa afya wa mara kwa mara na vipimo wakati mtumishi anapomaliza muda wake wa ajira kwa kustaafu, kuachishwa au kuhama.

“Madhumuni ya kufanya zoezi hili la ukaguzi wa afya ni kutaka kujua hali ya mtumishi kiafya”, alisema Dkt.Pricila.

Alibainisha aina ya vipimo wanavyohusika navyo kuwa ni pamoja na vya uzito, urefu, shikizo la damu, hali ya lishe na uwezo wa kuona mbali ili kujua hali ya afya ya mwajiriwa kwa ujumla na mazungumzo na Daktari.

Mkaguzi wa Afya wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA), Peter Kilimuhano alisema watumishi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania walipe kipaumbele zoezi hili la upimaji wa afya kwa kuwa ni muh9mu kwa afya zao.

Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) ni chombo cha kusimamia usalama na afya mahala pa kazi kwa kuhakikisha kwamba waajiri wote nchini wanaweka miundo na mifumo inayohakikisha usalama na afya mahala pa kazi vinalindwa.  

Posted in

Leave a comment