Na Mwandishi Wetu

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba amewataka watumishi wa Hazina ndogo mkoani Kigoma kufanya kazi kwa bidii, maarifa, weledi na kuzingatia kanuni katika majukumu yao.

Wito huo aliutoa wakati wa mazungumzo na watumishi hao alipotembelea Mkoa huo hivi karibuni ambapo alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Hazina ndogo.

Alisema kufuatia juhudi zinazofanywa na serikali katika kuboresha mazingira ya kazi na namna bora ya kuwahudumia wananchi wake watumishi hao wanatakiwa kufanya kazi kiueledi.

“Serikali inafanya kazi kubwa kwa kuweka mazingira wezeshi kwa watoa huduma na kuboresha miundombinu katika sekta zote ili wananchi wapate huduma bora kwa wakati na bila upendeleo” Dkt. Nchemba.

Mkuu wa Hazina Ndogo Mkoa wa Kigoma, Frank Msaki aliishukuru  serikali kwa kazi kubwa katika Kanda ya Kigoma kuhakikisha huduma muhimu zinapatokana kwa wananchi na kwa wakati.

“Sisi wasaidizi wake, tutaendelea kutoa huduma kwa kufuata misingi ya haki na uwajibikaji”, alisema Msaki..

Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mkoa wa Kigoma, Beatus Nchota alisema usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato katika Mkoa wa Kigoma unatokana na mwitikio mkubwa wa walipa kodi kufuatia elimu ya mlipa kodi wanayoitoa mara kwa mara kwa wafanyabiashara wa Mkoa huo.

Posted in

Leave a comment