Na Vincent Mpepo, Dodoma

Wakristo wametakiwa kuendelea kumtolea Mungu kwa ukarimu, uaminifu na moyo wa kupenda kama sehemu ya wajibu wao kwani kila wanachokimilki ni mali yake na wamepewa ili kuvitunza kwa faida yao na kwa utukufu wake.

Hayo yamesemwa na Mtheolojia Neema Swai wakati akihubiri katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Iringa Road, jijini Dodoma leo huku akibainisha kwamba hata wakitoacho ni sehemu ya mali ya Mungu.

Alisema utoaji ni tendo la ibada na si suala la kiuchumi pekee hivyo ni wajibu wa kila mkristo kujitathimini katika utoaji wake.

“Katika utoaji hatupotezi wala kufirisika bali tunapanda mbegu itakayotoa tija zaidi”, alisema Mtheolojia Neema.

Akizungumzia faida za utoaji alisema kutoa kunasaidia wahitaji kupata mahitaji yao na hivyo kujenga jamii inayojaliana na kuthaminiana.

“Kupitia utoaji mahitaji ya ndugu zetu wahitaji yanatimizwa na hivyo kuwa na jamii bora yenye kupendana yenye baraka za Mungu”, alisema Mtheolojia Neema.

Aliongeza kuwa, utoaji ni njia ya kufungua milango ya baraka za Mungu katika maisha yao na kujiwekea akiba kwao wenyewe na wanaonufaika na utoaji huo kupitia programu mbalimbali ikiwemo udiakonia.

Aidha aliwataka wakristo kutoenda kinyonge wakati wa kumtolea Mungu kwa kuwa wanamjua wanayemtolea na kwamba wanajua wanachokifanya na faida zake kimwili na kiroho.

Katika ibada hiyo huduma mbalimbali zilifanyika ikiwemo mnada wa bidhaa na vitu mbalimbali kwa ajili ya ujenzi wa kanisa, maombi na maombezi kwa ajili ya washarika na hususani wanafunzi wanaojiandaa na mithani ya Taifa inayotarajia kufanyika siku chache zijazo.

Posted in

Leave a comment