

Na Mwandishi wetu, Ruvuma
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Brigedia Jenerali Ahmed Abbas amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kufuatia utoaji wa mgari 24 kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni vitendea kazi muhimu vitakavyosaidia utekelezaji wa majukumu ya jeshi hilo.
Shukrani hizo alizitoa Septemba 16,2025 kwenye hafla fupi ya kukabidhi magari 24 iliyofanyika kwenye viunga vya Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoani Ruvuma yaliyotolewa na Serikali kwa Jeshi la Polisi mkoani humo.
Alisema anatambua thamani ya mchango huo kwa jeshi hilo kuwa magari hayo yatawarahisishia katika utendaji wa kazi ndani ya jeshi hilo huku akiwataka madereva kuyatunza magari hayo ili yadumu na kuendelea kutumika katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi.
“Magari haya ili yaendelee kufanya kazi kwa muda mrefu ni lazima yatunzwe kwa hali na mali”, alisema Brigedia Jenerali Ahmed
Aidha aliwataka aliwataka askari kufanya kazi kwa weledi, utii na kufuata Sheria za nchi kwani ndio kiapo cha askari wanachopaswa kuishi nacho katika majukumu yao ya kila siku na si vinginevyo.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Kamishna Msaidizi Mwandanizi wa Polisi, (SACP) Marco G. Chilya ameishukuru serikali na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (CPF) Camillus Wambura kwa kuona umuhimu wa kutoa magari hayo ambayo katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi Mkuu wa 2025.
Alaisema magari hayo pamoja na shughuli zingine yatasaidia kwa kiasi kikubwa katika shughuli za kulinda usalama wa raia na mali zao na kuhahidi kuwa magari hayo yatatumika kikamilifu kuimarisha na kudumisha amani ya Nchi.
Aidha alibainisha kuwa magari hayo yamekabidhiwa kwa wakuu wa vitengo ikiwa ni jitihada za serikali katika kuliwezesha Jeshi la Polisi kupata vitendea kazi vitakavyorahisisha utendaji wa majukumu yake ikiwemo kufanikisha usafiri na kufika kwa haraka kwenye maeneo ya matukio hususan katika kipindi hiki cha uchaguzi.

Leave a comment