
Na Vincent Mpepo
Wakuu wa idara, wakurugenzi na maafisa udhibiti ubora katika taasisi za elimu ya juu nchini za umma na binafsi wameelezea fursa na changamoto za matumizi ya akili mnemba (AI) katika taaluma huku wito ukitolewa kwa serikali, vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kuwekeza katika eneo hilo.
Hayo yamebainishwa na washiriki wa wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Jukwaa la Wadhibiti Ubora wa Taasisi za Elimu ya juu nchini (TUQAF) uliofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania jijini Dar es salaam.
Akiwasilisha mada katika mkutano huo, Profesa Justin Urassa wa Chuo Kikuu Cha Sokoine Cha Kilimo (SUA), alisema kutokana na maendeleo ya sayansi na teknnojia suala la udhibiti wa elimu kwa ngazi zote kuanzia ngazi ya awali hadi katika vyuo vikuu linapaswa kuzingatiwa.

Alibainisha baadhi ya namna za kudhibiti ubora wa elimu ikiwa ni pamoja na kuimarisha umahiri wa taasisi za elimu ya juu kwa kuwasomesha wahadhiri ili waendane na mabadiliko haya ya elimu ambayo yanabebwa na kasi ya maendeleo ya sayansi na teknolojia ikiwemo matumizi ya akili mnemba.
“Elimu ya juu ndiyo injini ya elimu katika ngazi zote, hivyo lazima iangaliwe kwa jicho la kipekee”, alisema Profesa Urassa.
Mkurugenzi wa Ubora wa Kurugenzi ya Uratibu Ubora Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan (JUCO), Dkt.Susan Kolimba alisema maendeleo ya sayansi na teknolojia hususani matumizi ya akili mnemba yana nafasi mbili katika jamii na katika taasisi za elimu ya juu.
Alisema uzoefu unaonesha kuwa matumizi ya akili mnemba kwa wanafunzi ni mabaya kutokana na kukosa ufahamu wa namna ya kutumia licha ya kukiri kuwa uvivu, kutojiongeza na kutojituma kunakotokana na uelewa duni wa athari za kufanya hivyo.
“Matumizi ya akili mnemba yanaweza kuwa ni fursa nzuri iwapo itatumika na kuratibiwa vizuri kwa wanafunzi na wahadhiri”, alisema Dkt.Kolimba.
Aidha, alisema kuwa ujio wa teknnolojia ya akili mnemba umekuwa ni kitu ambacho kimetokea bila maandalizi kwa taasisi za elimu ya juu hususani barani Afrika na kwingineko duniani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU), Dkt Francis Bigambilana alisema umefika wakati ambapo matumizi ya teknolojia ya akili mnemba yanapaswa kuweklewa vigezo vya udhibiti ubora vya ndani na nje katika mitaala na nyanja zote za ufundishji, ujifunzaji na usomaji katika taasisi za elimu ya juu ili viweze kupimwa.

Mkutano huo wa wa siku mbili wa jukwaa la wadhibiti ubora wa taasisi za elimu ya nchini ulihudhuriwa na wakurugenzi, wakuu wa idara na maafisa udhibiti ubora wa taasisi za elimu za juu za umma na binafsi nchini.
Leave a comment