Na Vincent Mpepo

Imeelezwa kuwa wanaume katika jamii wanapaswa kujitafutia furaha na kujifungamanisha na familia zao ili waishi maisha mazuri yatakayowaongezea maisha marefu na kuwapunguzia msongo wa mawazo na changamoto za afya ya akili na kupunguza vifo vyao ikilinganishwa na wanawake.

Hayo yamebainishwa na washiriki wa semina ya wanaume kwa njia ya mtandao iliyofanyika 16/09/2025 ikiratibiwa na Kitengo cha Jinsia cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kushirikiana na wadau.

Akiwasilisha mada katika mjadala huo, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania Mstaafu, Profesa Elifas Bisanda alielelezea dhana ya uhusiano uliopo kati ya mwanamke na mwanaume kibiblia na kihistoria akibanisha wazi kuwa mgawanyo wa majukumu kati ya mwanamke na mwanaume ulijulikana huku mwanaume akipewa nafasi ya maamuzi kwa masuala muhimu ya kifamilia tofauti na ilivyo sasa.

Alisema baadhi ya mila, desturi na tamaduni za kiafrika zinazohusisha mwanaume kutoa mahari wakati wa kuoa zinatajwa kuwa zilimpa nguvu na mamlaka mwanaume dhidi ya mwanamke huku matarajio ya jamii ni kuwa mwanaume ndiye chanzo cha mafanikio katika familia.

“Matarajio yaliyojengeka ilikuwa mwanaume ndiye anatarajiwa alete mafaniko katika nyumba, akifeli yeye basi nyumba yote imefeli”, alisema Profesa Bisanda.

Alisema wakati dunia imeingia katika maendeleo ya usasa masuala mengi yamebadilika na jambo muhimu la kuliangalia ni namna mtoto wa kiume anavyochukuliwa, kulelewa na anaandaliwaje kuja kuwa mume, mwanaume au mtu mwenye kufanya maamuzi.

“Tunamzungumzia mtoto wa kiume katika karne ya 21 na namna uwekezaji ulivyofanywa umejikita zaidi katika kumwezesha mtoto wa kike kuliko wa kiume”, alisema Profesa Bisanda.

Akizungumzia fursa ya elimu kwa mfano uwepo wa shule nyingi za michepuo mbalimbali za wasichana kuliko za wavulana na kubainisha kuwa hiyo ni dalili mbaya dhidi ya maandalizi ya mtoto wa kiume.

“Athari za kufanya hivyo ni kuwakatisha tamaa Watoto wa kiume na kujiona hakuna anayewajali na matokeo yake wengi huishia kwenye matumizi ya madawa ya kulevya, michezo ya kubahatisha na kamari”, alisema Profesa Bisanda.

Mhadhiri wa Sheria kutoka Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Ally Abdallah alizungumzia nadharia mbalimbali zilozoelezea nafasi ya mwanaume katika jamii huku zikionmesha wazi kuwa alipewa majukumu makubwa na mamlaka makubwa kutokana na uwezo wake mkubwa wa kutafuta rasimali za familia.

“Hakuna nadharia zinazoonesha ushahidi wa kisayansi zinazoonesha mwanaume kuwa mwenye nguvu na mamlaka katika familia”, alisema Dkt.Abdallah.

Alisema wakati huu wa karne ya sasa wanaume wanapaswa kubadilika kifikra kutokana na mabadiliko ya kimfumo ambayo yanatoa nafasi sawa kwa mwanamke na mwamanume huku wote wakiwa na uwezo kuzalisha na kutoa mchango katika familia tofauti na wakati uliopita ambapo mwanamke alipewa nafasi ya msaidizi au

“Nafasi ya mwanamke ambayo ilitazamwa hapo awali kama nmsaidizi, tegemezi kwa sasa haipo tena”, alisema Dkt. Abdallah

Alisema athari za mabadiliko hayo yaliyotokana na wanawake kupata fursa ya elimu, wakapata ajira na uwezo wa kiuchumi na nafasi mbalimbali ndiyo chanzo cha migogoro na wakati mwingine kuvunjika kwa ndoa nyingi kutokana na mtafaruku wa kimawazo.

“Majukumu ya ujinsia yataendelea kuwa kwa mujibu wa kibaiolojia ambayo yanampa mwanamke uwezo wa kubeba mimba, kuzaa na yanayofanana na hayo”, alisema Dkt.Abdallah.

Alisema majukumu ya kijamii kama kufua, kupika na shughuli mbalimbali ambayo kwa nyakati zilizopita yalionekana kuwa ni ya mwanamke kwa sasa yanapaswa na wote kwa kushirikiana kati ya mwanamke na mwanaume.

Kwa upande wake, Mshauri Mwandamizi wa Kiufundi wa Mpango katika Masuala ya Jinsia, Ngono, Ulinzi wa Mtgoto, Ndo na Masuala ya Afya Familia, Dkt.Katanta Simwanza alizungumzia umuhimu wa kuangalia masuala ya jinsia kwa umakini kwa sabau ndio yamekuwa ni chanzo cha changamoto nyingi katika maisha ya sasa.

“Hakika ya kweli iliyoko wanaume wengi hapa duniani wanatangulia mbele ya haki kwa sababu ya masuala ya kijinsia”, alisema Dkt.Katanta.

Alisema kuna faida kubwa sana ya kushirikiana kati ya mke na mume katika familia na faida zake ikiwemo kuwa na maono ya pamoja na wakati mwingine mwanamke kuwa msimamizi mkuu wa rasilimnali za familia.

“Kwenye familia nyingi ambazo wameweza kushikiana na kuheshimiana kwa kuwekeana kanuni wameweza kuona faida nyingi zaidi”, alisema Dkt.Katanta.

Alisema ni muhimu kwa kila familia kuwa na sera, mingozo na taratibu za kuzisimamia ambazo zinatoa nafasi ya wajibu na majukumu kwa kila mwanafamilia.

Semina maalumu kwa wanaume iliandaliwa na Kitengo cha Jinsia cha Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya MBS Trinity Care ikiwa na malengo ya kuchochea uelewa kuhusu nafasi ya wanaume katika uwezeshaji wanawake na kuvunja mitizamo hasi, kujenga ushirikiano wa kijinsia na kuhamasisha wanaume kuwa mabalozi wa mabadiliko chanya katika jamii.

Semina hiyo  ilioongozwa na Mtangazaji na Mwandishi wa Habari kutoka Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Njwaba Mwaijibe ni miongoni mwa mojawapo iliyovuta makini ya washiriki na kuibua hisia tofauti miongoni mwa washiriki kitu kinachoonesha kuwepo kwa changamoto ambayo ihahitaji kuwepo kwa hatua za makusudi miongoni mwa na jamii hususani katika malezi na makuzi ya mtoto wa kiume.

Posted in

Leave a comment